Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa |
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi anayeshughulikia elimu, Kassim Majaliwa, alipokuwa akizungumza na watumishi wa manispaa ya Tabora.
Majaliwa ambaye alikuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya elimu mkoani Tabora, alisema malalamiko mengi yaliyotolewa na walimu yalionyesha kuwa maofisa elimu wamekuwa hawawajali.
Alisema sio maofisa elimu tu, hata watu wa masijala nao wamekuwa wakitumia lugha mbaya wanapowahudumia watumishi hali ambayo imekuwa ikizusha malalamiko toka kwa walimu na kusababisha wasifanye kazi yao kwa ufanisi.
"Mjenge tabia ya kuwaheshimu watumishi wa serikali wakiwemo walimu, kwani serikali imeshusha majukumu kwenu wakurugenzi wa halmashauri na maofisa elimu, hivyo tumieni nafasi zenu kumaliza kero za watumishi," alisema.
Aliongeza kuwa ni aibu maofisa elimu na wakurugenzi kulalamikiwa na walimu kuwa wanatumia lugha mbaya pale wanapowahudumia na kwamba tabia inafanya serikali ichukiwe kwa makosa ambayo ni watu wachache.
Alifafanua kuwa siyo kila tatizo la mtumishi wa serikali lipelekwe wizarani wakati viongozi hao wapo, akawataka kila mmoja kufanya kazi ipasavyo kwenye eneo lake badala ya kuwa chazo cha matatizo.
Aidha, aliwataka wakuu wa shule kuwa na vipindi vya kufundisha badala ya kufanya kazi za utawala tu huku shule zao zikikabiliwa na uhaba wa walimu ambao unachangia wanafunzi kukosa baadhi ya masomo.
Alisema kuwa karibu shule zote alizotembelea alikuta zina uhaba wa walimu na kwamba serikali inaendelea kutatua tatizo hilo ambapo mwaka huu imeajiri walimu zaidi ya 20,000 ambao wamepangwa kwenye shule mbalimbali nchini.
Alisema kuwa mshikamano kati walimu na wakuu wao utasaidia kuleta maendeleo kwenye maeneo yao wanayofanyia kazi badala ya malalamiko ambayo yanachangia kurudisha maendeleo nyuma.
Mbali na hayo, Naibu Waziri aliwataka walimu na wazazi kukomesha utoro wa rejareja kwa wanafunzi ambao umezikumba shule nyingi mkoani humo na kusababisha wengi wao kufanya vibaya kwenye mitihani yao.
0 Comments