Daniel Mjema, Dodoma na Editha Majura, Dar

KITENDO cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kushindwa kuzungumzia shinikizo la baadhi ya wabunge kutaka mawaziri wanane wajiuzulu, kimeonekana kuwakera wawakilishi hao ambao sasa wameamua kuibana Serikali huku wakiapa kukwamisha bajeti za mawaziri hao katika Bunge lijalo la Bajeti.

Juzi walianza kuonyesha makali baada ya kukataa mapendekezo ya Mfumo wa Mpango wa Mabadiliko wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 wakisema hauna jipya na umetayarishwa kwa mfumo uleule kwa miaka 15 mfululizo.

Majuzi, Pinda aliahirisha Bunge bila kugusia shinikizo la wabunge hao kutaka Serikali iwawajibishe Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika.

Wakizungumza na kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao, wengi wao wakiwa ni wa CCM, walisema silaha pekee waliyobaki nayo ni kukwamisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013 katika kikao kijacho cha Bunge.
Wabunge hao pia wameonya kwamba kutojiuzulu kwa mawaziri hao kutaiweka CCM njia panda katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwani hoja ya ufisadi ndiyo iliyowafanya wenzao wengi wasirudi bungeni.
“Silaha kubwa tuliyobaki nayo sasa ni kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na nakuambia kama ile karatasi ingerudi upya leo idadi ya wabunge wa CCM ambao wangetia saini ingetikisa nchi,” alisema James Lembeli wa Kahama (CCM).
Lembeli alisema anashangaa kuona mawaziri waliotakiwa kujipima wenyewe na kuandika barua za kujiuzulu wakigoma kufanya hivyo na Serikali kupuuza hoja hiyo akisema, hatashangaa kuona Watanzania wakiingia mitaani.
“Kitendo cha Waziri Mkuu kutosema chochote kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri hao wakati akihitimisha Bunge ni kuiingiza nchi kwenye mgogoro mkubwa. Serikali ifahamu kuwa, ipo madarakani kwa ridhaa ya wananchi,” alisema.
Lembeli alisema wananchi walipokea kwa shangwe taarifa ya mawaziri hao kutakiwa kujiuzulu lakini, kitendo cha Waziri Mkuu kuwaacha na kuikwepa hoja hiyo alipokuwa akiahirisha Mkutano wa Bunge juzi, kitaongeza chuki ya wananchi dhidi ya Serikali yao kwa kuwa wataamini inawakumbatia mafisadi.
“Inakuwaje hawa mawaziri wanane tu watake kuitumbukiza nchi kwenye machafuko? Uwaziri ni dhamana aangalie huko kwenye vijiwe na mitaani watu walivyoshangilia kusikia wametakiwa kujiuzulu leo wanagoma, unamgomea nani?” alihoji Lembeli.
Lembeli alisema anaamini Rais atafanya uamuzi mgumu na wa haraka kabla ya Bunge la Bajeti vinginevyo Waziri Mkulo na mawaziri wengine watakuwa na wakati mgumu ambao haujawahi kuonekana katika kupitisha bajeti za wizara zao.
Mbunge mmoja wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM kutoka Kanda ya Ziwa, alisema ukimya wa Rais Kikwete na kiburi cha mawaziri wake wenye tuhuma za kweli kugoma kujiuzulu, kumezidi kukifanya chama hicho tawala kuporomoka umaarufu.



Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema Rais Kikwete anapaswa kuheshimu maoni na maelekezo ya wabunge na kusema hata kutaka mawaziri wajiuzulu ni utaratibu tu wa kistaarabu.
“Sisi Wabunge 76 tuliosaini hoja ya kutaka Waziri Mkuu ang’oke tumejitoa sadaka kwa maslahi ya nchi lakini naamini wakati wa kumpigia kura Waziri Mkuu, wengi zaidi watatuunga mkono kwa jinsi walivyokerwa na jambo hili,” alisema.

“Bunge safari hii limeisha kimyakimya, Spika alipowahoji wanaoafiki hoja ya Waziri Mkuu ya kuliahirisha Bunge waliosema siyo ndiyo waliokuwa wengi na kama ulifuatilia Bunge lilikuwa kimya si kawaida… Rais anatakiwa alione hilo,” alisema.
Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM), alisema amesikitishwa na hatua ya mawaziri hao kugoma kujiuzulu na kwamba kwa hali ilivyo, busara ya kawaida inataka mawaziri hao wajiuzulu.
“Kwa busara ya kawaida wote wanaotuhumiwa kwa wizara zao kufanya madudu wangeacha uroho wa madaraka na kujiuzulu ili kuitikia kilio cha wabunge na Watanzania kwa sababu upepo huko nje sio mzuri hata kidogo,” alisema Azzan.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) alisema taifa limeghafilika kwa sababu wananchi wengi nchi nzima walikaa kwenye luninga na kusikiliza redio juzi jioni wakitarajia Waziri Mkuu angetamka moja kwa moja kuwang’oa mawaziri hao.
“Jana kwenye baa na vijiwe ilikuwa kama vile kuna mechi ya kukata na shoka... kwa jinsi idadi kubwa ya wananchi walivyofuatilia hotuba ya Waziri Mkuu lakini mwisho wa siku akawaacha solemba,” alisema.
Nape, Mukama

Baadhi ya wabunge wa CCM waliosaini barua ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wamedai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Mukama amewatisha.

Kanji Lugola wa Mwibara alidai jana kwamba usiku wa kuamkia Jumapili, siku moja baada ya kusaini hati hiyo alipokea simu kutoka kwa Mukama akimtolea maneno makali kutokana na hatua yake hiyo.

“Alizungumza maneno mengi ya vitisho kwa mfululizo bila hata kunipa nafasi ya kujieleza, akasema, ‘nakuja huko wewe na huyo mwenzako mliosaini mtanitambua,’ kuona hivyo tukaondoka Dodoma usiku huohuo,” Lugola alieleza.

Alisema walisafiri hadi Dar es Salaam na kwamba walihudhuria kikao cha Bunge cha Jumatatu iliyopita wakitokea mafichoni.Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo Mukama alisema: “Siwezi kutoa habari kwa simu.”

Alipopigiwa tena na kuombwa afuatwe ofisini alisema, “Kwa leo haitawezekana maana niko njiani natokea Dodoma sasa hivi nimefika Gairo, kama unaweza njoo kesho.”

Lugola alidai wakati akipokea vitisho hivyo kutoka kwa Mukama waliokuwa wamesaini kwa upande wa CCM walikuwa yeye na Filikunjombe, baadaye alifuatia na Nimrod Mkono.

“Kinachofanya tufikie hatua hii ni kutoridhishwa na dhamira ya dhati ya chama chetu katika kuisafisha Serikali… na ieleweke kuwa hatuna mpango wa kuhama chama chetu kwa kuwa lengo letu ni kukiimarisha,” alisema.

Akizungumzia madai hayo ya vitisho, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye alisema wabunge hao hawana hatia kwani msimamo wao ni sehemu ya kutekeleza wajibu wao.

Alisema ingawa hakuwa na taarifa za vitisho dhidi ya wabunge hao, CCM hakijafanya kikao chochote kuzungumzia suala hilo na kusema kama kuna mtu aliyewatisha basi amechukua hatua zake binafsi.

“Wabunge wana haki ya kuhoji utendaji wa Serikali yao na hata kuiwajibisha, hakuna mwenye haki ya kuwabagua kiitikadi, kiimani wala kikabila hivyo wanaojadili suala hili kwa misingi ya kibaguzi hawawatendei haki…, wanataka watekeleze vipi majukumu yao?”

Alisisitiza kuwa ndiye msemaji wa CCM hivyo ieleweke kuwa kilichofanywa na wabunge si uasi na jamii isiwagawe kwa namna yoyote ile bali, matendo yao ndani ya Bunge yaheshimike kwa mujibu nyadhifa zao.

Waanza kuonyesha makali
Wabunge waliyakataa mapendekezo ya Mfumo wa Mpango wa Mabadiliko wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 wakisema hauna jipya na umetayarishwa kwa mfumo uleule kwa miaka 15 mfululizo na kwamba vigezo vyote, uchumi wa Tanzania unakuwa kwa viwango visivyoridhisha na ukuaji huo hauendi sambamba na kasi ya kupunguza umasikini na kukuza pato la mwananchi wa kawaida.

Mpango huo ulioandaliwa na Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha uliwasilishwa jana kwenye Kamati ya Mipango ya Bunge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Abdallah Kigoda alisema mfumo huo unahitaji mabadiliko ili uendane na wakati uliopo ikiwamo kutoa majibu ya tatizo la mfumuko wa bei.

“Mapendekezo yanayotayarishwa yanajikita zaidi kwenye eneo la maelekezo badala ya maagizo. Lazima Serikali itoe majibu kuwa sera za fedha na kodi zinatakiwa ziweje ili kujibu tatizo la mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi.” alisema Dk Kigoda.

Mbunge huyo wa Handeni (CCM), alisema mapendekezo hayo hayajaeleza kwa kina namna sekta ya fedha itakavyosaidia katika kutatua tatizo la uhaba mkubwa wa mitaji unaohitajika kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.

“Hivi sasa tunazo takriban benki 45 na taasisi kadhaa za fedha lakini bado wananchi wengi hawajapata fursa ya kutumia huduma za kifedha katika shughuli zao za kuibua mapato yao na kupata ajira,” alisema.

Katika mapendekezo hayo ya kamati, Dk Kigoda alitaka kutumika kwa sheria mpya ya madini, kampuni za simu zitozwe kodi kama inavyofanyika katika nchi nyingine za Afrika na kodi za majengo.

Alisema mpango huo ulipaswa kujikita katika kuagiza namna ya kudhibiti matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri nyingi na ubainishe usimamizi wa fedha na kuagiza ni hatua gani zichukuliwe ili kupunguza matumizi mabaya ya fedha.

Wabunge walichangia mpango huo waliupinga. Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Kessy alisema anapata hofu ya taifa kujikuta likiomba fedha za misaada kutoka nchi ya Cameroon kwa kushindwa kukusanya kodi.

Alishangaa Serikali katika mpango huo kuelezea kuongeza uzalishaji wa matunda wakati haina uwezo wala kuzalisha matunda huku akiponda hoja ya kwamba itaimarisha viwanda wakati yenyewe ndiyo iliyoviua.

Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliishangaa Serikali kujivunia kuwa nchi ina amani na usalama wakati haina usalama kutokana na watu kuwa na njaa... “Hakuna vita mbaya kama taifa kuwa na watu wenye njaa. Tatizo la mfumuko wa bei hasa katika vyakula ni kubwa kutokana na kutokuwepo kwa uthibiti wa bei hizo.”

Akiwasilisha mpango huo, Wassira alitaja baadhi ya maeneo ya kipaumbele kwa mwaka 2012/2013 kuwa ni miundombinu, uzalishaji na usambazaji umeme, barabara, kilimo, viwanda, utalii, huduma za kifedha na tekinolojia ya habari na mawasiliano.

Wassira alisema ili kupunguza pengo katika bajeti ya maendeleo na pia kuchochea kasi ya utekelezaji wa mpango wa mwaka na kutekeleza miradi ya kimkakati, itailazimu Serikali kukopa mikopo maalumu kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Kwa kuanzia katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, Serikali itahitaji kukopa Dola za Marekani 540 milioni sawa na Sh864 bilioni mahsusi kwa ajili ya kusaidia uwekezaji wa kimkakati kwa sekta binafsi ili iweze kuwekeza katika miradi ya maendeleo.

Zitto: Sasa tunajipanga
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amesema baada ya Pinda kugoma kuwachukulia hatua mawaziri hao, chama chake sasa kinajipanga kufanya mazungumzo na vyama vyote ambavyo wabunge wake walitia saini kukubaliana na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu huyo ili waone namna ya kuitisha maandamano nchi nzima.

“Lazima Watanzania waelewe suala la kutaka mawaziri hawa wajiuzulu si la Wabunge wa Chadema wala la Zitto, hili ni la wabunge wote isipokuwa UDP na nyinyi ni mashahidi kuwa waliopiga kelele sana ni wabunge wa CCM. Sasa tunafanya mazungumzo na vyama vilivyounga mkono hoja hiyo ili tupange kwa pamoja ni kwa namna gani maandamano hayo yanapaswa kufanywa,” alisema na kuongeza:

“Tunataka kumwambia Rais Kikwete kuwa gharika inakuja na asitafute mchawi ni ama awaondoe mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi na utendaji mbovu au wakumbane na Tsunami ya nguvu ya umma.”



                                          CHANZO CHA HABARI HIZI NI HAPA