IDADI kubwa ya wagonjwa waliokwenda kutafuta tiba kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile, Loliondo wamepoteza maisha.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo sasa itatangaza matokeo ya utafiti wa tiba hiyo ya ‘Kikombe cha Babu’ imesema wengi ni wale wenye Ukimwi walioacha matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs).
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli, aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jana Dar es Salaam, kwamba hadi sasa Serikali inafanyia utafiti watu 206 ambao walipata kikombe hicho.
Utafiti unaofanywa na Wizara hiyo inataka kubaini kama kweli dawa hiyo ina uwezo wa kuponya Ukimwi, kisukari, saratani na magonjwa mengine sugu. Wanaofanyiwa utafiti huo walipata ‘kikombe’ hicho baada ya kuugua kisukari na Ukimwi.
“Kwa sasa ni vigumu kusema dawa hiyo inaponya au haiponyi, tusubiri utafiti wa kitaalamu. “Baada ya miezi miwili tutatangaza matokeo kwa umma,” alisema Kikuli na kuongeza kuwa utafiti huo unafanywa katika hospitali mbalimbali nchini chini ya usimamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Utafiti huo unafanywa katika hospitali za Bugando, Mwanza; Mbeya; Mount Meru, Arusha; Hydom, Manyara na KCMC, Kilimanjaro. Hospitali hizo ziko maeneo ambayo wananchi wengi walijitokeza kupata ‘kikombe’ Loliondo. Kikuli pia alisema kwa sasa idadi ya Watanzania wanaokwenda Loliondo kupata tiba hiyo imepungua; lakini bado wananchi wa kutoka Kenya na nchi zingine wanaendelea kwenda kupata ‘kikombe’ hicho.
Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Donan Mmbando, alikiri kuwa wagonjwa wengi wa Ukimwi waliokwenda kupata tiba hiyo na kuachana na ARVs wamepoteza maisha. Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy Mohamed (CCM), aliishauri Wizara hiyo kuacha siasa badala yake iwaambie wananchi kwamba dawa ya Babu wa Loliondo haina madhara kwa binadamu, lakini pia haina uwezo wa kuponya magonjwa.
“Msiogope kusema kama wanasiasa, ninyi ni wataalamu, ni kweli kuwa ile dawa haina madhara kama yalivyo maji, lakini tusidanganyane, haitibu, kwa nini mnaendelea kudanganya wananchi?” Alihoji Mbunge huyo. Makamu Mwenyekiti wa PAC, Zainab Vullu, ndiye aliyetaka Wizara itoe taarifa ya utafiti wa tiba ya ‘kikombe cha Babu’.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alitaka kujua kama bado kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaokwenda kupata tiba hiyo Loliondo. Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola, alitaka kujua kama Wizara hiyo imewasiliana na nchi zingine za Ulaya ambazo raia wake walikwenda kupata tiba ya ‘kikombe’ kama walipona magonjwa waliyokuwanayo.
“Wenzetu wale Wazungu ni wepesi katika masuala haya ya utafiti, nataka kujua kama mmefanya juhudi za kuwasiliana nao?” Alihoji mbunge huyo na kujibiwa na Kaimu Mganga Mkuu kuwa kila nchi ina utaratibu wake wa utafiti.
Wakati huo huo, Wizara hiyo imeendelea kushutumiwa na wabunge hao kuwa inalipa mishahara hewa wafanyakazi ambao wameshafariki dunia na ambao wameacha au kuachishwa kazi, hivyo kuingiza hasara Serikali.
Pia wabunge hao walihoji hatua zinazochukuliwa na Wizara baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuonesha kuwa kuna maofisa wa Wizara hiyo wanaoghushi barua za kujipandishia mishahara kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Hazina.
Mbunge wa Chwaka, Yahya Khamis Issa (CCM), ndiye aliyehoji suala hilo na kujibiwa na Kaimu Katibu Mkuu kuwa masuala ya malipo hewa na udanganyifu wa mishahara bado yanafanyiwa kazi na wizara yake ili kuhakikisha hayajitokezi tena.
Nanenane yagharimu bilioni 2/- Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeihoji Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii sababu za kutumia zaidi ya Sh bilioni 1.9 kwa sherehe za Nanenane.
Fedha hizo zilitumika kulipa posho watumishi wa wizara na taasisi zake wapatao 350, ununuzi wa suti, fulana na chakula kwa wataalamu waliotoa huduma kwa wagonjwa katika maonesho hayo yaliyofanyika hadi usiku.
Pia katika fedha hizo kulijengwa banda la maonesho lililogharimu Sh milioni 386 ambalo baada ya kumaliza maonesho walilikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa matumizi mengine.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, aliitaka Serikali kuangalia umuhimu wa maonesho hayo yanayogharimu fedha nyingi na matumizi mengine ambayo hayakupitishwa na Bunge.
Alisisitiza kuwa ifike mahali Serikali iangalie tija ya maonesho hayo na gharama zinazotumika, huku baadhi ya sekta muhimu zikikabiliwa na upungufu wa fedha, kama ukosefu wa dawa na matumizi mengine katika kukuza sekta ya afya. Awali, Kikuli alidai fedha hizo zilitumika kwa maadhimisho ya Nanenane Dodoma baada ya kupata maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu.
Alisema pia walichangisha taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo na kupata Sh milioni 76 kwa ajili ya maonesho hayo zilizoongezwa na zingine ambazo walizitumia kugharimia maonesho hayo.
Akizungumzia suala la pango la jengo la Wizara hiyo, Mhasibu Mkuu wa Wizara, Hellen Mwakapunga alisema wanalipa Sh milioni 200 kwa mwezi kwa ajili ya pango la Wizara na taasisi zingine za chini yake.
Alisema jengo la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii linalipa Sh milioni 32 kwa mwezi huku wakiwa na deni la Sh milioni 800 kwa ajili ya pango katika Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Lakini alisema awali kiwanja chenye jengo hilo kilikuwa cha Wizara ambapo kulikuwa na mkataba wa kujenga jengo lingine lakini wanashangaa kuendelea kulipa kodi kwa miaka mingi, huku umiliki ukihamishiwa NHC.
Kamati hiyo iliiagiza wizara kuhakikisha inarejesha jengo hilo chini ya umiliki wake, kwa kuangalia mkataba wa awali, kuhusu ujenzi wa jengo hilo ili kuokoa mabilioni ya fedha wanayolipa posho na kuingia katika huduma nyingine.
Akijibu tuhuma hizo, Meneja Huduma kwa Jamii wa NHC, Muungano Saguya, alisema jengo hilo ni la NHC kwani Msajili wa Majumba miaka ya nyuma alipewa na Serikali kiwanja hicho na kuagizwa kujenga jengo kwa ajili ya kukodisha Wizara ya Afya.
Alisema kiwanja hicho namba 36 na 37 kilichopo mtaa wa Samora kilihamishiwa katika umiliki wa NHC kama sheria ilivyoagiza. *Imeandikwa na Shadrack Sagati na Theopista Nsanzugwanko.
0 Comments