BAADHI ya wabunge wametaka Serikali kufuta ajira za mikataba kwa watumishi waliofikia umri wa kustaafu hasa kwa fani zenye wataalamu wengi nchini ili kutoa fursa kwa vijana wenye sifa na uwezo wa kupata ajira.

Wabunge hao walidai kuwa utaratibu huo unafanya vijana wengi wanaohitimu vyuoni kukosa ajira na kufanya idadi ya watu wasio na ajira kuongezeka nchini.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia alitetea utaratibu huo kuwa unafanywa kwa watumishi wa kada za elimu na afya kutokana na mahitaji yao na wakati huo huo kuendelea kuongeza udahili wa wataalamu katika fani hizo ili kutosheleza mahitaji.

Ghasia alisema siyo sera ya Serikali kuajiri kwa mkataba watumishi waliostaafu na kama inavyobainishwa katika waraka wa Rais namba moja wa mwaka 1998.Hata hivyo, alisema inapothibitika kuwa utaalamu wa mstaafu husika bado unahitajika na hakuna mtumishi mwingine anayeweza kufanya kazi alizokuwa akizifanya, wanampa mkataba mstaafu huyo kwa manufaa ya umma.

Ghasia alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Sara Msafiri (CCM). Waziri huyo alisema Serikali humwomba mhusika kuendelea kufanya kazi kwa mkataba wa kipindi maalumu.

Hata hivyo, jibu hilo halikuwaridhisha baadhi ya wabunge na ndipo aliposimama Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM) na kudai kuwa ana ushahidi kuwa wapo wastaafu waliopewa mikataba ya ajira katika fani ambazo zina wataalamu wengi nchini.

“Naomba Serikali ieleze inatumia utaratibu gani katika kutoa mikataba hii maana wapo wastaafu wengi wameongezewa mikataba wakati tunao vijana wengi kwenye fani hizo,” alihoji Munde ambaye pia alitaka umri wa kustaafu kwa hiari upunguzwe hadi miaka 50 na kwa lazima iwe miaka 55. 
Ghasia katika kujibu swali hilo alisititiza kuwa mikataba hiyo inatolewa hasa kwenye sekta ya elimu na afya ambako kuna idadi ndogo ya walimu na madaktari na sio vinginevyo.

Kuhusu umri wa kustaafu, Ghasia alisema miaka 55 watumishi wengi wanakuwa bado vijana hivyo kuweka sheria hiyo kwa sasa itafanya watu wengi wahudumiwe kwenye pensheni na hivyo kuweka mzigo mzito kwenye eneo hilo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), yeye alihoji kama Serikali imedhamiria kuondoa tatizo kwa vijana kwa nini inapotangaza nafasi zake nyingi inaweka na vigezo vya uzoefu wakati vijana wanaohitimu vyuoni hawana uzoefu wa kazi.

“Huyu kijana tunataka akatoe wapi uzoefu wakati ndio kwanza kahitimu kutoka chuo kikuu?” alihoji Bulaya. Ghasia alisema sio kweli kuwa Serikali katika kazi zake zote inaweka vigezo vya uzoefu badala yake akasema kuwa tatizo liko kwa vijana wenyewe ambao wakishahitimu shahada ya kwanza au ya pili anataka akaanze kazi akiwa mkurugenzi.

Alisema kuna kazi za kada za chini Serikali hutangaza nafasi za kazi bila kuweka kigezo cha uzoefu ila wanaweka uzoefu kwenye kazi za ukurugenzi au ofisa mwandamizi ambao wanaotakiwa ni lazima wawe na uzoefu wa kazi. “Ni kweli kuna kazi zinazohitaji uzoefu lakini sio zote, hakuna kazi ya kuanzia juu lazima vijana wetu waingie katika mlango sahihi kwenye ajira,” alisema Ghasia.