Na Mwandishi Wetu
MWIGIZAJI ‘hot’ wa filamu za Kibongo, Jacqueline Masawe ‘Wolper’, amewaziba midomo baadhi ya mastaa wenzake wakiwemo Wema Sepetu na Irene Uwoya kufuatia hivi karibuni kuanika vielelezo vya uthibitisho kuwa gari la kifahari analotanulia jijini ni mali yake halali.
Wolper alifikia hatua hiyo baada ya kukerwa na maneno yaliyozagaa mitaani kuwa vitu vingi alivyonavyo sasa, likiwemo gari aina ya BMW X6 lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 170 ni mali ya mchumba wake hivyo hatakiwi kuringa.
Akizungumzia ishu hiyo juzikati, Wolper alisema amekuwa akiumizwa na maneno hayo kwani hayana ukweli wowote na yamekuwa yakilenga kumchafua.
“Hao wanaosema hili gari ni ‘gari funguo’ wanakosea na hawanijui vizuri, mimi ni tofauti na wasanii wengine. Siwezi kutembelea gari ambalo siku yoyote naweza kupokonywa, hili ni langu na hati ninazo (akizionesha), sasa sijui huko waliko wanasonyaje?” alisema Wolper na kuongeza:


“Nilidhani kwa mafanikio niliyoyapata wenzangu watanipongeza lakini kumbe inawauma na wengine kukimbilia kusema eti naringa na ipo siku nitasafiri kwa daladala, maneno gani sasa hayo kama siyo kuvunjana moyo?”
Hivi karibuni Wolper alibadili dini na kuitwa Ilham baada ya kupata mchumba Muislam aliyemtaja kwa jina la Dulla ‘Dallas’ ambaye alimnunulia gari sambamba na kumboreshea maisha.
 Katika uchunguzi wetu, tumebaini kuwa gari analotumia Wolper kwa sasa lilinunuliwa Sh. milioni 115 huko Uingereza na gharama za kuliingiza Bongo ni Sh. milioni 60 hivyo kulifanya liwe na thamani ya shilingi milioni 175.
Mbali na gari hilo, Wolper ana magari mengine mawili ambayo ni Toyota Harrier Lexus lenye thamani ya Sh. milioni 25 ambalo linatumika kuwapeleka wadogo zake shuleni.
Pia Wolper anamiliki Toyota Noah lenye thamani ya Sh. milioni 18 analolitumia kwenye kazi za filamu chini ya kampuni yake ya Dallas Entertainment.
Inaaminika kuwa ndiye staa wa kike anayemiliki gari la bei mbaya zaidi Bongo ukilinganisha na ‘mahasimu’ wake, Wema anayemiliki Toyota Harrier Lexus ya Sh. milioni 25 na Uwoya anayesukuma Toyota Fortuner ya Sh. milioni 60.