Sifael Paul na Issa Mnally
KIFO cha kiungo mshambuliaji wa Timu ya Simba ya Dar es Salaam, Patrick Mutesa Mafisango kimetonesha kidonda cha marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ kufuatia kuibuka kwa mapya ya kushangaza.
Tayari Chanzo cha habari kimeshapokea malalamiko kutoka kwa mashabiki wa soka Bongo kuwa mastaa wa filamu hawakuonesha ushirikiano kwenye kifo cha Mafisango kama wachezaji wa soka na michezo mingine walivyofanya kwa Kanumba.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili ambao hawakuwa tayari majina yao yaandikwe, walisema kuwa wakati wa kifo cha Kanumba ‘kampani’ kutoka katika michezo ilikuwa kubwa kuliko walivyofanya watu wa maigizo kwenye kifo cha Mafisango.
JINSI YA KUWALILIA
Wakati hayo yakiendelea, Amani limeelezwa kuwa kuna utofauti mkubwa wa jinsi wachezaji walivyopokea habari za kifo cha Mafisango na kuwa hata namna ya kumlilia ilikuwa tofauti na walivyofanya mastaa wa filamu kwa Kanumba.
Ikadaiwa kuwa katika msiba wa Mafisango, wanasoka wengi wa kiume hata wale ambao siyo wa Simba walishuhudiwa wakishindwa kujizuia na kuangua kilio hadharani tofauti na wasanii wa filamu wa kiume ambao hawakuonesha majonzi mazito kwenye msiba wa Kanumba.
Aidha, ilielezwa kuwa kwa Mafisango waliokuwa wanalia kupita maelezo ni wanaume tofauti na ilivyokuwa kwa marehemu Kanumba ambapo waliokuwa wakilia na kuzimia ni wanawake na ilifikia hadi hatua ya mwanamke mmoja mkoani Pwani kunywa sumu baada ya kusikia taarifa za kifo cha mwigizaji huyo.
“Ina maana kiwango cha uvumilivu baada ya kutokea kwa kifo cha mtu kwa wacheza sinema ni kikubwa kuliko kwa wacheza mpira?” alihoji mtoa habari mmoja aliyezungumza na gazeti hili.
MASUTI
Mtoa habari wetu akazidi kuweka ushahidi wake hadharani kama hivi:
“Kwa Mafisango hakukuwa na ‘masuti’ kama yale ya akina JB (Jacob Steven). Zaidi sana, wachezaji mavazi yao na wale wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ walibeba mwili wa marehemu Mafisango wakiwa na jezi zao walizotokanazo kambini.
Wala hakukuwa na mtu aliyekuwa anakenua msibani kama walivyofanya waigizaji kwenye Viwanja vya Leaders Kinondoni (Dar) wakati wa kuaga mwili wa marehemu Kanumba.”
HURUMA YA WASANII
Mtoa habari huyo akazidi kusema: “Hivi huruma ya wasanii wa Bongo Movie kwa Kanumba ilikwenda wapi maana walionekana kama wenye nyuso zisizo na huzuni! Kusema kweli walisikitisha sana.
“Wewe mtu utapewaje taarifa ya kifo cha msanii mwenzako uliyekuwa ukifanya naye kazi muda mwingi halafu unaanza kutafuta suti hadi za kukodisha?
“Mbona akina Boban (Haruna Moshi) walifika kwenye msiba wakiwa kawaida tu na wala hakukuwa na miwani myeusi kama kwenye msiba wa Kanumba.
“Inawezekana kabisa waigizaji waliponzwa na umaridadi kwani ulitawala sana wakitaka kujionesha wao ni nadhifu.”
Amani lilipozungumza na baadhi ya mastaa wa Bongo Movie kuhusu ishu hiyo kila mmoja alitoa utetezi wake, wengine hawakutaka kabisa kusikia habari hiyo.
Hata hivyo, kumbukumbu inaonesha kuwa baadhi ya mastaa wa kiume wa Bongo Movies walidondosha machozi alfajiri ya kifo cha Kanumba, hasa walipokuwa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Msanii Single Mtambalike ‘Richie’ alipopigwa picha na mapaparazi, alionekana kwenye kamera hospitalini hapo akiwa anajipigapiga kichwa kwa kutoamini kilichotokea.
0 Comments