Mwendesha mashtaka mkuu mpya katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), Fatou Bensouda, amesema wababe wa kivita wanawatisha viongozi wanaojaribu kuwatia mbaroni.
Bi Bensouda ametoa wito kwa viongozi wa Afrika wasikubali kutishwa na viongozi kama vile jenerali muasi Bosco Ntaganda.
Akizungumza na BBC, Bi Bensouda amesema kuwa wababe hao wanawatisha viongozi kuwa ikiwa hawata legeza kasi ya kuwasaka basi wataendelea kuwaua watu.
Katika siku za hivi karibuni, mamia ya watu wameuawa huko mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo wanajeshi wanamsaka Jenerali Ntaganda.
Mwezi March mwaka huu, mahakama ya ICC ilimpata mshirika wake mkuu wa Jenerali Ntaganda, Thomas Lubanga na hatia ya kutekeleza uhalifu wa kivita mashariki mwa Congo.
Bi Bensouda ambaye ni wakili kutoka Gambia ni mwaafrika wa kwanza kuteuliwa kama mwendesha mashtaka katika mahakama hiyo.
Ataanza kutekeleza majukumu yake mwezi ujao baada ya kustaafu kwa Louis Moreno Ocampo.
0 Comments