BAADA ya mwaka 2005 kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kubwagwa katika hatua za awali, Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, kwa mara nyingine ametangaza kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015.

Shibuda alitangaza azma yake hiyo juzi mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwenye semina iliyofanyika Dodoma katika ukumbi wa Nec ya CCM iliyojadili hali ya utawala bora nchini iliyotolewa na taasisi inayotathmini utawala bora Afrika (APRM).

Shibuda ni mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo anayewakilisha vyama vya upinzani.

"Nakupa pole, kazi ya urais ni ngumu sana, bila shaka utakumbuka kuwa nami nilitaka kuwa mbadala wako, hata hivyo naamini utakuwa meneja wangu wa kampeni za urais mwaka 2015," alisema Shibuda.
Huku wajumbe wa NEC wakishangalia, Rais Kikwete alimwuliza: "unataka urais kupitia chama gani?" Shibuda akajibu kwa kujiamini: "Kupitia Chadema, huku niliko sasa”.

Kauli ya Shibuda imekuja wakati kukiwa na minong'ono ya baadhi ya wanasiasa wazito ndani ya chama hicho kutaka kuwania nafasi hiyo.



Wanasiasa wanaotajwa kutaka kwa udi na uvumba kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema, ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Mbunge wa Hai Freeman Mbowe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa ambaye aliwania mwaka 2010.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa NEC Shibuda alisema kwa kuwa mwaka 2005 aliomba ridhaa ya CCM kugombea urais akakosa nafasi hiyo alimwomba Rais Kikwete awe mpiga debe wake na kuamini kuwa kwa kazi nzuri aliyofanya nchini kwa kipindi cha miaka aliyokaa madarakani, akimpigia debe bila shaka atafanikiwa.

Kikwete akamwuliza anataka ampigie debe kupitia chama gani? Shibuda akajibu “kupitia Chadema,” wajumbe wa NEC wakamshangilia kwa nderemo na vigelegele.

Shibuda pia alizungumzia nafasi ya CCM katika siasa ya Tanzania, na kusisitiza kuwa hivi sasa hakuna mbadala wa CCM katika kuongoza nchi.

Alisisitiza kuwa CCM imejijenga kimfumo kuanzia ngazi ya juu mpaka mashinani, jambo ambalo linarahisisha utoaji haki kuanzia chini mpaka juu.

Mbunge huyo, alisisitiza kuwa tatizo ndani ya CCM ni baadhi ya viongozi kuwa wabinafsi ambao aliwafananisha na kunguru wasiofugika, kwa kutofuata miiko na maadili ya chama na badala yake kuwa sehemu ya watu wanaoharibu chama hicho.

Hata hivyo, alisema pamoja na yote, bado nafasi ya CCM kuendelea kuongoza Dola ni kubwa, kwani mpaka sasa vyama vya siasa vya upinzani, bado havijawa na uwezo wa kutekeleza chochote zaidi ya CCM.