Jeshi la Uganda linasema kuwa limemkamata afisa mwandamizi wa kundi la wapiganaji la LRA - kundi ambalo limekuwa likiwauwa na kuwateka nyara watu Afrika mashariki na ya kati, kwa zaidi ya miaka 20.Kiongozi wa LRA, Joseph Kony anasakwa na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa, kwa uhalifu wa vitani.
Washauri wa Marekani wamekuwa wakisaidia majeshi ya nchi za Afrika mashariki na kati katika msako wao wa kumtafuta Kony pamoja na wafuasi wake.
Jeshi la Uganda linasema limemkamata kamanda mwandamizi wa LRA, Caesar Achellam kando ya Mto Mbou katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Limesema Achellam alikuwa na bunduki tu ya aina ya AK-47 na risasi chache.
Ingawa LRA inasemekana kuwa na wapiganaji mia mbili-tatu tu, hata hivo imeleta maafa nchini Uganda, Sudan Kusini, Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa kuuwa na kuwatesa watu, pamoja na kuwateka nyara watoto wao na kuchoma moto nyumba zao.
0 Comments