CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka wazi masuala kitakayotetea kuwa katika Katiba mpya huku kikiruhusu wananchi kuamua kuhusu masuala ya madaraka ya Rais na uteuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Sisi CCM tumeona suala hili tuwaachie wananchi walijadili na kuamua wenyewe wanaona Rais apewe madaraka ya aina gani. Ni fursa yao kupendekeza apunguzwe, aongezwe madaraka au madaraka yake yaweje,” alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Katika eneo la Tume Huru ya Uchaguzi, Nape aliyezungumza na vyombo vya habari jana, alisema eneo hilo limekuwa gumzo hasa nyakati za uchaguzi huku malalamiko mengi yakiegemea katika utaratibu uliotumika kuteua wajumbe wa Tume hiyo.

Alisema mapendekezo hayo yaliamuliwa katika semina ya wajumbe wa NEC kuhusu mchakato wa Katiba mpya iliyomalizika hivi karibuni Dodoma.

“Chama kimeona suala hilo lijadiliwe na wananchi na wapendekeze utaratibu mwafaka wa kuteua Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema Nape.
Alitaja masuala mengine ambayo chama hicho kimeona wapewe wananchi fursa ya kuchangia maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi na ikiwezekana yabadilishwe, kuwa ni masuala yanayosababisha kero za Muungano na utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Uteuzi wa mawaziri Alitaja pia maeneo ya kujadiliwa kuwa ni eneo la uteuzi wa mawaziri, waziri mkuu, muundo wa Bunge, Baraza la Wawakilishi na aina ya wabunge na wawakilishi, kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais ambapo kwa sasa, mfumo hauruhusu suala la mgombea binafsi.



“Kuna watu wanadhani kuwa CCM inaogopa mgombea binafsi, si kweli, hatuna tatizo na hilo na ndiyo maana tumeliweka hili watu walijadili na kuamua watakavyo, ingawa kwa mtazamo wangu, mgombea binafsi ni kitanzi kwa upinzani,” alisema.

Aidha alitaja maeneo mengine kuwa ni uwepo wa Baraza la pili la Kutunga Sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi wa Serikali ya Muungano na mfumo wa Mahakama.

Pia chama hicho kilitoa mapendekezo yake juu ya masuala ya msingi yanayofaa kuingizwa kwenye Katiba, kuwa ni pamoja na maadili ya viongozi kupewa nguvu kikatiba na Serikali kuendelea kuwa mmiliki mkuu wa rasilimali zote za nchi.

Katika masuala ya msingi ya kuingizwa katika Katiba yaliyopendekezwa na chama hicho, ilikuwa suala la maadili ya viongozi kuingizwa na kutambuliwa kikatiba ili kudhibiti wabadhirifu na wasio na maadili, kwa kuwa kwa sasa hata Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi haina meno ya kutosha kama inavyotarajiwa.
“Kutokana na yaliyotokea juzi ya mawaziri kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma, ni vema suala hili la maadili likajengewa nguvu ya kikatiba, kuliko ilivyo sasa lakini pia sera ya sasa ya Serikali kuwa mmiliki wa rasilimali kuu za nchi, iendelee hususan eneo la ardhi,” alisisitiza.

Serikali mbili Aidha, alitaja maeneo mengine ambayo chama hicho kimependekeza yaingizwe kwenye Katiba mpya kama msimamo wake, kuwa ni kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuendelea kubaki na muundo wa serikali mbili ya Muungano na ya Zanzibar.

“Serikali mbili ndiyo sera ya CCM, tumejadili na kuona haina upungufu, ila ukumbi uko wazi kwa wanaoona tofauti kutoa maoni yao kwa Tume ya Kukusanya Maoni kwa ajili ya Mchakato wa Katiba Mpya,” alisema.

Alitaja maeneo mengine yaliyopendekezwa kuingizwa kwenye Katiba mpya kuwa ni kuendelea na mihimili mitatu (Serikali, Bunge na Mahakama), kuendelea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na umoja wa kitaifa, amani, utulivu, usawa na haki.

Maeneo mengine aliyotaja ni kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara katika vipindi maalumu na kuzingatia haki ya kupiga kura.

“Eneo hili limetujengea heshima kidemokrasia, kwani kuna nchi ambazo marais wao wako madarakani muda mrefu na hawataki kuondoka.”

Katika kipengele cha uchaguzi mdogo alisema CCM ilishatoa msimamo wake, ambapo ilipendekeza inapotokea mbunge amefariki dunia au kung’olewa madarakani kisheria, chama kilichokuwapo madarakani kipewe nafasi ya kuteua mrithi wake kama inavyofanyika sasa kwa wabunge wa viti maalumu. “Tulishasema hili tukaambiwa CCM tunaogopa uchaguzi mdogo.”
Aidha, Nape alitaja maeneo mengine ya kuingizwa kwenye Katiba, kuwa kuendeleza uhifadhi na ukuzaji wa haki za binadamu, kuheshimu usawa mbele ya sheria, kuendeleza sera ya Dola kutokuwa na dini rasmi na kuruhusu kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoitaka.

Maeneo mengine ni kuimarisha madaraka ya umma, kuhamasisha sera ya msingi wa kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine maalumu katika jamii, kusimamia hifadhi ya mazingira na kuendelea kuwapo kwa Rais Mtendaji.

Nape alisema mapendekezo hayo yataandaliwa kimaandishi na kukabidhiwa kwa Tume ya Kukusanya Maoni kwa ajili ya Mchakato wa Katiba Mpya na masuala ya kujadiliwa yatapelekwa kwa wanachama wa chama hicho ili waweze kujiandaa kuchangia.