Na Waandishi Wetu
WAKATI wakiwa nchini India kwa matibabu, huku nyuma nyumbani kwa mastaa wanandoa wa filamu za Kibongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ (pichani) na Wastara Juma kumeibuka mkasa mpyaa, Ijumaa lina ripoti ya kusikitisha.
Kwa mujibu wa Wastara, wakiwa katika Hospitali ya Saifee iliyopo jijini Mumbai nchini humo, walipokea taarifa mbofumbofu kutoka nyumbani kwao Tabata Barakuda, Dar es Salaam kuwa kuna matapeli waliojifanya waganga walifika kwenye familia wakitaka kumtibu Sajuki ilihali wakijua ameshapelekwa India.

TATIZO
“Kuna tatizo limetokea huko nyumbani Tanzania, kuna matapeli wanaifuata familia, wanajifanya ni waganga, wanataka kumtibia Sajuki,” ilisomeka sehemu ya maelezo ya Wastara aliyoyatuma kwa Mtangazaji wa Clouds FM, Dina Marios.
Wastara alieleza kuwa watu hao walitaka wapewe Sh. milioni
3.5 ili wamuokoe Sajuki kwa sababu kalogwa na mtu aliyemdhulumu hivyo ugonjwa wake siyo wa kwenda kutibiwa India.
“Ukweli sisi hatujawahi kumdhulumu mtu. Waganga hao wapo wengi wanaisumbua familia tangu tulipoondoka.
“Naomba waache hiyo tabia si nzuri kwani wanatukwaza sana,” alisema Wastara, kauli iliyowatoa machozi Watanzania kwa mara nyingine kwani hadi akafikia hatua hiyo ina maana hali hiyo imewaumiza.

MATIBABU
Tofauti na ilivyokuwa ikiripotiwa kuwa Sajuki alikwenda kutibiwa katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi, India, Wastara alisema wapo katika Hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai, India na madaktari walikuwa wakiendelea na vipimo.
“Tulifika salama, wamerudia tena vipimo ili wajue waanzie wapi,” alisema Wastara.

KINACHOMTESA SAJUKI
Kinachomtesa mwigizaji Sajuki ambaye pia ni prodyuza wa filamu ni uvimbe pembeni ya ini kitaalam ni dalili za ugonjwa wa Hepatoma (kansa ya ini).

KILA LA HERI SAJUKI
Timu ya Ijumaa na Wafanyakazi wa Kampuni ya Global Publishers, wanawatakia Sajuki na Wastara kila la heri katika safari yao ya matibabu nchini India.
Tunaamini watarejea na matumaini tele kwani tunasubiri kuwaona runingani wakituburudisha tunapokuwa sebuleni kwetu hivyo wanaokwenda nyumbani kwa mastaa hao na kujaribu kuingiza mambo yao waache mara moja.