Raymond Kaminyoge na Zaina Malongo MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa leo wanatarajiwa kuhutubia wanachama na mashabiki wa chama hicho katika mkutano mkubwa uliopangwa kufanyika katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Mbowe alisema jana kwamba mkutano huo unalenga pamoja na mambo mengine, kuwaandaa kisaikolojia wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kukipokea chama chake kuingia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alijigamba kwamba Chadema hakina shaka kwamba kitashinda Uchaguzi Mkuu ujao na kuunda Serikali, hivyo kinapaswa kuwaandaa watu kisaikolojia. Huu ni mkutano mkubwa wa kwanza wa Chadema kufanyika Dar es Salaam baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010. Unafanyika kipindi ambacho wapenzi na wanachama wake wakiwa bado wanasherehekea ushindi wa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika katika hukumu ya kupinga matokeo yake ya ubunge iliyotolewa juzi na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa wameruhusu kufanyika kwa mkutano huo, lakini wakazuia maandamano kutokana na kile alichodai kuwa ni kutokuwa na askari wa kutosha.
Vuguvugu la Mabadiliko Mbowe alisema katika mkutano huo, viongozi wa chama hicho watawaeleza wananchi namna Programu ya ‘Movement for Change’ (Vuguvugu la Mabadiliko) inavyofanya kazi.
Alisema Chadema kimeanzisha Programu ya Movement for Change ili kuwahamasisha wananchi kujiunga na chama hicho na kuendeleza maono ya kuusaka uongozi wa nchi mwaka 2015. Pia alisema kwamba mkutano huo utatumika kuzindua rasmi mpango wa kitaifa wa kukichangia chama hicho, ili kujenga uwezo wa kujiendesha sasa na siku zijazo. “Tutawaeleza wananchi wawe tayari kwani chama chao kina kila sababu ya kushika dola katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015. Pia wafahamu nini wanachotakiwa kufanya kwa sasa katika maandalizi hayo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunataka wananchi, Watanzania wawe sehemu ya mabadiliko tunayoyakusudia kuyafanya katika nchi yetu, wawe wamiliki wa mabadiliko hayo. Sasa watashiriki vipi? Ndiyo jambo tunalokwenda kuwaambia kesho.” Katika hatua nyingine, Mbowe alisema viongozi wa Chadema watatumia fursa hiyo kuwaeleza wanachama na wafuasi wao msimamo wa uongozi katika upatikanaji wa Katiba Mpya.
“Tutazungumzia pia jukumu la chama na wananchi katika kuharakisha upatikanaji wa Katiba Mpya na maandalizi ambayo chama kimeyafanya,” alisema. Mbowe alisema katika mkutano huo, pia watazungumzia hali ya uchumi na mfumuko wa bei ambao umekuwa ukisababisha maisha ya wananchi kuwa magumu siku hadi siku. Katika siku za karibuni, Chadema kimekuwa kikilaani kupanda kwa gharama za maisha na kusema kwamba hali hiyo imekuwa ikisababishwa na baadhi ya vigogo wa Serikali kuishi maisha ya anasa na ufisadi.
Maandamano
Kuhusu kuzuia maandamano, Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba wameyazuia kufanyika kwa maandamano ya chama hicho akisema polisi imebaini uwezekano wa uvunjifu wa amani kama yataruhusiwa.
Awali, Chadema kiliandaa maandamano hayo kikitaka yawe sehemu ya mkutano wake na juzi, katika matangazo yake, kilisema wafuasi na wapenzi wake watafika Jangwani kwa maandamano kutoka mitaa mbalimbali kwa kuwa hawana nauli za kupanda daladala. Lakini Kamanda Kova alisema licha ya kudai wafuasi hao wa Chadema hawana nauli, jeshi limepinga maandamano yao na kuwataka wanaotaka kuhudhuria mkutano huo wasikubali kuandamana.
“Hawaruhusiwi kufanya maandamano. Ruksa kufanya mkutano wao kwenye Viwanja vya Jangwani, lakini wanatakiwa kuhakikisha utulivu katika mkutano huo,” alisema Kova na kuongeza: “Tumewapa kibali cha kufanya mkutano na siyo kibali cha maandamano. Yeyote atakayeshiriki maandamano yaliyopangwa na Chadema ajue amevunja sheria na polisi haitasita kumchukulia hatua.”
Akizungumzia hatua hiyo ya polisi, Mbowe alisema: “Bado tunaendelea kufanya mazungumzo na polisi, lakini kama wakishindwa kutuelewa basi, hatutalazimisha.” “Nimesema kwamba hata hivyo, hayakuwa maandamano kwa mtindo wa fikra walizonazo polisi, tunaweza kuyaita matembezi ya hamasa.
Tulitaka watu wetu wasio na uwezo wa kupata nauli wajiunge kwenye makundi watembee hadi Viwanja vya Jangwani.” Alisema mtizamo huo ulizingatia ukweli kwamba wananchi wengi hawana uwezo wa kupata nauli kutoka wanakoishi hadi Jangwani na kwamba waliamini kwa kuwa kwenye makundi wangeweza kufika katika viwanja hivyo na kushiriki mikutano.
0 Comments