Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Idd Simba akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana baada ya kusomewa shtaka la kudanganya, kugushi na kuliingizia hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 2 Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Mshtakiwa huyo alipata dhamana. (Picha na Yusuf Badi).
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba, Meneja Mkuu Victor Milanzi na mjumbe Salim Mwaking'inda, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka saba, yakiwamo ya kujipatia Sh milioni 320 za shirika hilo kinyume cha sheria.
Vigogo hao wa Uda walisomewa mashitaka yao jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ben Lincon mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta, na baada ya kukana mashitaka waliachiwa kwa dhamana.
Washitakiwa hao waliachiwa baada ya kutimiza masharti yaliyowataka kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni 500 kila mshitakiwa na kutoa mali isiyohamishika ambapo Simba alitoa hati ya kampuni ya Keys.
Mashitaka ya kwanza kusomwa yalihusu kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu ambapo ilidaiwa kwamba Septemba 2, 2009 Simba na Milanzi walitenda kosa hilo.
Katika mashitaka ya pili ambayo ni ya kughushi, Simba na Milanzi siku hiyo hiyo Dar es Salaam wanadaiwa kughushi barua ya tarehe hiyo ikionesha kuwa akaunti za Uda zilitolewa fedha zaidi ya zinazoruhusiwa kisheria.
Pia wanadaiwa kwamba kwa kutumia nyadhifa zao na kwa manufaa yao waliingiza fedha kwenye akaunti ambayo haikudhamiriwa, wakati fedha hizo zilitakiwa kuwa malipo ya awali ya hisa za Uda ambayo ni Sh milioni 320.
Katika mashitaka ya nne, Simba na Milanzi wanadaiwa kujipatia Sh milioni 320 kutoka kwa Robert Kisena, fedha ambazo zilikuwa malipo ya awali ya ununuzi wa hisa za Uda.
Pia Simba na Milanzi wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya, kwani kati ya Septemba 3, 2009 na Machi 31, 2010 Dar es Salaam, walijipatia Sh milioni 320 fedha ambazo zilikuwa sehemu ya malipo ya hisa za Uda na kusababisha hasara hiyo.
Katika mashitaka ya sita, washitakiwa wote watatu wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya, kwa kuwa siku zisizofahamika Septemba 2009 na Februari 2011, walitumia madaraka vibaya kwa kuuza hisa za kampuni hiyo ambazo zilikuwa hazijatolewa na Jiji la Dar es Salaam, ambaye ndiye mmiliki wake akishirikiana na Serikali Kuu.
Washitakiwa hao katika mashitaka ya saba wanadaiwa kutumia madaraka vibaya ambapo walidhamiria kutoa hisa ambazo hazijatolewa na Uda bila kuhusisha Serikali.
Kwenye mashitaka ya mwisho ya kusababisha hasara, wanadaiwa kulisababisha hasara shirika la umma kiasi cha Sh 2,378,858,878.80.
Simba alipata kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiongozwa na Benjamin Mkapa, kabla ya kupata kashfa ya sukari iliyomng’oa uwaziri huo.
Mwaking’inda alipata kuwa diwani wa kata ya Sinza wilayani Kinondoni na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam huku pia akiwa kiongozi wa Chama cha Soka Kinondoni (Kifa).
Naye alipata kutajwa katika kashfa za viwanja katika wilaya hiyo na hatimaye kuangushwa katika kinyang’anyiro cha udiwani katika uchaguzi Mkuu mwaka juzi.
0 Comments