Ndugu zangu,
Leo asubuhi niliweka picha na maelezo ya Balozi wetu nchini Ubelgiji, Mh. Diodorus Kamala akiwa hapa Msamvu, Morogoro.

Haraka sana kuna waliokimbilia kumwita Kamala fisadi na majina mengine. Hapa kuna tatizo kwetu Watanzania, kwamba kila mtu ni fisadi na hasa akiwa kada wa Chama Cha Mapinduzi.

Nadhani hatutendi haki kwa kukimbilia kuwahukumu watu bila ushahidi. Na Kamala niliyemjua sasa ni wa kupigiwa mfano kwa staili yake ya maisha. Naweza kusema, kuwa Kamala ni Mjamaa mwenzangu kutokana na msimamo wake kiitikadi na staili yake ya maisha.

Ukweli ni huu, hapa Msamvu Kamala na mimi, tangu jana tumeishi kwenye nyumba moja ya wageni ambayo gharama ya chumba chake kwa usiku mmoja haizidi shilingi elfu 30. Na hapo unapata chai ya nguvu asubuhi. Ni mahala pazuri, pametulia na unapata huduma nzuri kama uko nyumbani.

Siwezi kabisa kuamini, kuwa Kamala ana utajiri wa kutisha uliotokana na kutumia nyadhifa zake alizowahi kuzipata. Na kama ana utajiri mkubwa, basi, utakuwa ni wa kufuata ' masharti ya waganga wa kienyeji'. Maana, ile Nissan aliyoendesha asubuhi kwenda nayo Dar ina thamani inayokaribia na ' Kifaru' cha Mwenyekiti wenu ambacho wengine mnakiita ' Kibajaji'.

Umefika wakati kwa Watanzania wa kuacha kutoa hukumu za jumla na zenye kuwakandamiza wengine kutokana na itikadi zao, au vyama wanavyotoka. Maana, kama Kamala huyu huyu angeishi maisha haya na huku akiwa Chadema, basi, kuna wengi sana wangemsema vizuri na kumtolea mifano. Na tunasahau, kuwa hata kwenye vyama vya upinzani ikiwamo Chadema, yumkini kuna wabunge wanaoishi maisha ya kifahari ambayo Kamala hawezi kuyakaribia.

Nitazidi kumtetea Comrade Kamala mpaka pale nitakapojiridhisha kuwa ninayemtetea si Kamala huyu niliyemfahamu sasa.

Maggid Mjengwa,
Msamvu, Morogoro.
0788 111 765