Elvan Stambuli na Mitandao
MTOTO mmoja amezaliwa jijini Karachi nchini Pakistan akiwa na miguu sita na amefanyiwa upasuaji kuondoa iliyozidi.
Jopo la madaktari waliomfanyia upasuaji huo Alhamisili iliyopita kwenye taasisi iitwayo National Institute of Child Heath (NICH), jijini Karachi wamesema upasuaji ulikwenda vizuri kama walivyopanga.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Dk. Jamal Raza ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa NICH, alisema miguu mingine iliondolewa kwa operesheni na hali hiyo hutokea mara chache sana.
“Kati ya watoto milioni moja, anaweza kutokea mmoja tu kukumbwa na hali hiyo kutokana na maradhi ambayo kitaalamu huitwa Genetic Disease. Mtoto huwa si wa kawaida,” alifafanua Dk. Raza.
Alisema mtoto huyo kabla hajafanyiwa upasuaji alipimwa na kipimo maalum, CT Scan ndipo walipoamua kumfanyia upasuaji uliochukua saa nane.
Baba wa mtoto huyo ambaye hajapewa jina, Imran Shaikh, alisema ameshukuru mtoto wake kupata tiba hiyo na sasa amekuwa kama watoto wengine. “Sisi ni maskini, naishukuru serikali kwa kusaidia tiba ya mwanangu,” aliwaambia wanahabari.