KATIKA tukio lisilo la kawaida, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, juzi usiku alivamia katika Stesheni za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwanusuru abiria waliokwama kwa zaidi ya saa 12 katika stesheni kuu hiyo.

Abiria hao, wakiwemo wagonjwa na watoto, walikuwa wanasafiri na treni ya mamlaka hiyo kwenda mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya na nchi jirani ya Zambia.

Bila kutarajia Dk. Mwakyembe alifika katika stesheni hizo saa mbili na nusu usiku, ikiwa ni punde tu baada ya kurejea kutoka katika safari ya kikazi nje ya nchi na uvamizi wake ulizaa matunda baada ya treni hiyo iliyokuwa iondoke Dar es Salaam saa saba mchana kufanikiwa kuondoka saa sita usiku wa kuamkia jana.

Jitihada za Waziri Mwakyembe, zilileta matumaini mapya baada ya jitihada za uongozi wa TAZARA kugonga mwamba kwa kile kinachodaiwa ni kushindwa kumudu ununuzi wa mafuta ya treni (dizeli) kutokana na kukosa fedha.

Hatua hiyo inadaiwa kutokana na kampuni za mafuta zilizokuwa zikiiuzia dizeli mamlaka hiyo kusitisha huduma hiyo hadi pale TAZARA itakapolipa malimbikizo ya madeni.

Mgomo huo uliifanya TAZARA kufanya makubaliano na kampuni ya Lake Oil inayotoa huduma hiyo hivi sasa, ingawa nayo imetoa sharti gumu la kulipwa fedha taslimu ndio itoe mafuta.

Hali hiyo tete inaelezwa kuzifanya safari za abiria wa TAZARA zinazopaswa kufanyika Jumanne na Ijumaa kuwa za kubahatisha na zisizozingatia muda, kitendo kilichomfanya Waziri Mwakyembe atoboe siri kuwa uongozi wa juu wa mamlaka hiyo unahujumu safari hizo, na si uhaba wa fedha wala dizeli.

Alitoa maneno hayo juzi usiku baada ya kuwaokoa abiria zaidi ya 1,000 waliokuwa wamekwama katika stesheni hiyo wakisubiri kusafiri na treni hiyo katika vituo tofauti 65 vilivyopo kati ya Dar es Salaam na New Kapiri Mposhi.

HABARILEO Jumapili ilikuwepo katika eneo hilo hadi saa 6:20 usiku wakati treni hiyo ya abiria ilipoondoka na kumshuhudia Dk. Mwakyembe akiwaomba radhi abiria waliokuwa wakipiga kelele kwa hasira, wakiashiria kuchoshwa na uzembe unaofanywa na Menejimenti ya Mamlaka hiyo kuwaahirishia safari mara kwa mara bila kuwaeleza ukweli wa kilichopo.
Abiria hao wanawake, watoto, wanafunzi, wazee na watu wenye ulemavu, walionekana kutojali kukanyagana ilimradi wasogee karibu na Dk. Mwakyembe ili kusikia neno la matumaini au la kukatisha tamaa kuhusu safari yao iliyopaswa kuanza saa 7:50 mchana na baadaye kuahirishwa hadi saa 4:30 usiku kabla ya kuahirishwa tena hadi saa 6:20 usiku.

Huku wakilalamika kuharibiwa ratiba, abiria hao walisema mipango ya shughuli walizokuwa wakizifuata waendako zilikuwa zimetibuliwa na uzembe huo wa uongozi wa TAZARA.

Walisikika pia wakilalamikia bei ya huduma katika mgahawa ndani ya stesheni hiyo kwamba zipo juu na kusema huenda mgahawa huo ni wa mmoja wa viongozi wa TAZARA anayewacheleweshea safari ili wanunue vyakula vyake anavyoviuza kwa bei ya juu.

“Waziri anapaswa kuangalia pia kitega uchumi cha mgahawa wa humu ndani kuona kama si wa mhujumu mwingine wa TAZARA kwa sababu vyakula vinavyoshibisha vyenye bei ya chini vinaanzia Sh 5,000 kwa sahani, ambayo wengi tunaocheleweshewa safari kwa uzembe wao hatumudu kununua,” alisikika mmoja wa abiria.

Gazeti hili lilishuhudia idadi kubwa ya abiria wakila mikate, juisi na visheti huku watoto wachanga waliokuwa wakisafiri na mama zao wakikorogewa maziwa ya unga yaliyochanganywa na maji baridi ya uhai, kutokana na kushindwa kumudu gharama za vyakula.

Hasira ya Dk Mwakyembe Kutokana na hali halisi aliyoiona hapo stesheni na maelezo ya viongozi ‘aliowabana’ ili wamweleze kulikoni, Waziri huyo alionesha wazi kukasirishwa na ubabaishaji wa kiutendaji.

Aliweka bayana kuwa mabadiliko kwa uongozi wa juu wa TAZARA hayakwepeki na kwamba kamwe Serikali haitaichangia mamlaka hiyo fedha za kuisaidia kujiendesha, ikiwa itaendelea kubaki na viongozi wasio waaminifu.
“Mnajua nilikuwa nje ya nchi na nimerejea nchini leo na kupokewa na ujumbe mfupi wa simu ulioniarifu kuhusu kuahirishwa kwa safari ya leo ya abiria. Huu ni usumbufu na upuuzi usiovumilika. Naona hapa wengi wanaoteseka ni Watanzania waliolipa nauli mapema kabisa. Ikibidi watangazieni wajue kama safari ni usiku wa manane na si kuwachuuza.

“…Na kama mnaona hamuwezi si tuambiane ukweli tu wanaume wenzangu tujue kama tunaendelea au tunaachana na biashara hii?” Dk Mwakyembe aliwaeleza na kuwauliza viongozi wa TAZARA waliokusanyika kumsikiliza stesheni hapo bila uwepo wa Mkurugenzi wao Mtendaji (Mzambia), Akashambatwa Mbikusita -Lewanika aliyedaiwa kuwa amelala nyumbani kwake wakati huo, huku Naibu wake Damas Ndumbaro akielezwa kuwa safarini kikazi.

Akijibu maswali ya Dk Mwakyembe, Meneja Mkuu Mkoa kwa upande wa Tanzania, Abdallah Shekimweri alisema tatizo linalowasumbua zaidi ni ukosefu wa mafuta kwa ajili ya treni na tayari wamelipa Dola za Marekani 700,000 (Sh bilioni 1.2) ili kupata lita 75, 000 zitakazowasukuma kwa miezi ya usoni.

“Tatizo letu ni mafuta ya treni. Kampuni ya Lake Oil nayo imeanza kutaka fedha taslimu baada ya mkataba wao kwisha. Na leo ndio imetupa taabu zaidi kwa sababu wametaka hata fedha tuliyoipeleka benki waione kwanza kwenye akaunti zao ndio watupe mafuta. Ndio maana hadi usiku huu tunahangaika”.

Waziri alipotaka kujua ni kwa nini kampuni hiyo haijapewa mkataba hadi usiku ule alijibiwa na kiongozi huyo na wenzake wengine kuwa ulikuwa umekwamia kwa Mkurugenzi Mtendaji aliyepaswa kuusaini.

Wakati akizungumza na viongozi hao, abiria walikuwa wakipiga kelele wakiomba wapelekewe viongozi wa TAZARA ili wawashughulikie kwa kuwa hawakuwa na wema wala huruma kwao, hoja iliyopingwa na Dk Mwakyembe aliyewasihi watulie. “Tulieni matatizo ya TAZARA ninayashughulikia na ingekuwa ni uamuzi wangu kama Waziri wa Uchukuzi bila kusubiri kushirikiana na mwenzangu wa Zambia, sasa hivi ningefanya mabadiliko ya msingi…lakini si mbaya, tutakuwa na mkutano wa maana katika wiki mbili zijazo. Tutajua nini cha kufanya,” alisema.

Kadhalika, alielezwa juu ya kuwepo kwa urasimu mkubwa wa taarifa za fedha na manunuzi Makao Makuu inayowajumuisha watu wa ngazi ya Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Naibu Mkurugenzi na viongozi wachache wa juu.

“Unaotuona hapa hatujui chochote kuhusu fedha wala manunuzi mheshimiwa, tunaambiwa madaraka yetu hayafiki huko kwa hiyo tunachoweza kukwambia ni kwamba mafuta hatuna wala fedha za kuyanunulia ya kutosha kwa kipindi kirefu na pia hatujui ni kwanini mkataba wa anayetupa mafuta hausainiwi hadi haya yanatokea, ” alisema mmoja wa viongozi hao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Stesheni ya Dar es Salaam, Walivyo Maneno alisema siku hiyo ya safari ziliuzwa zaidi ya tikiti 1,000 ambapo abiria wa kukaa kwa mabehewa saba ya daraja la tatu ambayo yaliyokuwa yamejaa walikuwa zaidi ya 672. Kabla ya kuwa na abiria waliosimama, behewa moja linapakia abiria 96.