KIUNGO mchezeshaji wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango amefariki dunia usiku wa kuamkia jana Alhamisi katika ajali mbaya ya gari iliyotokea majira saa ya 9:30 usiku karibu kabisa na Chuo cha Ufundi Stadi cha Veta, Keko katika barabara ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo marehemu alikuwa na wenzake wanne akiwemo mpwa wake aliyefahamika kwa jina moja la Olilembe, Gasper aliyeumia bega, Bozii na mwanamke mmoja ambaye hajafahamika.
Gari aina ya Toyota Cresta lenye namba za usajili T 387 BMZ lilikuwa linaendeshwa na Mafisango baada ya kumpoka usukani Bozii.
Mara baada ya tukio hilo, Chanzo cha habari kilifika katika hospitali ya Muhimbili saa 12:09 asubuhi na kuushuhudia mwili wa mchezaji huyo ambapo kwa mujibu wa wahudumu wa mochwari, marehemu alifikisha hospitalini hapo saa 10 alfajiri.
Gazeti hili lilishuhudia mwili wa Mafisango ukiwa na majeraha makubwa ikiwamo kuchanika kichwani, kuvimba uso na jicho lake la kushoto kuingia ndani.

Kifo chake kimewashtua wengi, jijini Rwanda. Askari waliopima ajali hiyo, mmoja aliliambia gazeti hili kuwa inaonekana huenda gari alilokuwemo marehemu liligongwa nyuma kabla ya kupinduka.
Kauli hiyo inazua utata kwa kuwa maelezo ya kwanza yanaonyesha alimkwepa mwendesha pikipiki lakini gari linaonyesha kama limegongwa nyuma.

Majeruhi azungumza:
Akizungumzia kifo hicho, Olilembe alisema: “Tulikuwa tunatoka katika ukumbi wa Maisha (Maisha Club) uliopo Masaki. Tulikuwa tukiendeshwa na Bozii, lakini tukiwa njiani (hakumbuki wapi) marehemu aling’ang’ania aendeshe ndipo Bozii akaamua kumpisha.
“Tulipofika eneo la tukio, kuna pikipiki ilitokea mbele yetu ndipo Mafisango akawa anataka kumkwepa, katika kuhangaika akajikuta analipeleka gari kwenye mtaro wa pembeni. Yeye alifariki palepale, wengine hatukuumia sana, baada ya muda tulipata msaada, tukapelekwa Muhimbili.

Saa 10:00 alfajiri
Emmanuel Okwi na Derrick Walulya ndiyo wachezaji wa kwanza kufika Muhimbili na ndiyo ambao walikuwa wakisaidia kuubeba mwili wa marehemu kuuingiza mochwari, pamoja na kuwasaidia majeruhi.
Saa 1:07 asubuhi
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Tanga, Steven Ngonyani ‘Maji Marefu’ ambaye ni shabiki wa Simba aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo kutokana maradhi ya vidonda vya tumbo, akiwa na Kamanda Jamal Rwambow walikuwa viongozi wa kwanza kufika mochwari kushuhudia kilichokuwa kikiendelea.
Saa 1:49 asubuhi
Kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Bobani’ alifika mochwari, alishindwa kujizuia na kuanza kuangua kilio akitaka apewe nafasi ya kuuona mwili wa marehemu.
Muda mfupi badaye aliruhusiwa kuingia ndani akiongozana na kaka yake, mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Idd Moshi pamoja na beki wa zamani wa Simba, Said Kokoo kushuhudia mwili wa Mafisango. Wawili hao walitokea mlango wa nyuma na kuondoka.

Saa 2:54 asubuhi

Kiungo mchezeshaji wa Yanga, Haruna Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda na rafiki wa karibu wa marehemu, alifika muda huo akiongozana na Uhuru Selemani wa Simba, wote wawili walikuwa wakitokwa na machozi.
Niyonzima alisema: “Kifo cha Mafisango kimeishtua Rwanda akiwemo Kocha Mkuu wa Rwanda, (Sredojević) Micho. Tulitakiwa tuondoke pamoja leo kwenda Rwanda lakini yeye (Mafisango) akaniambia atachelewa kidogo angeondoka Ijumaa (leo).
“Nilipata taarifa za kifo cha Mafisango nikiwa uwanja wa ndege (Julius Nyerere) najiandaa kuondoka, nashindwa kuelewa sijui itakuwaje, nauomba uongozi wa Simba ufanye jitihada za kuusafirisha mwili wake kwa kuwa familia imeomba akazikwe nyumbani kwao.”
“Nahisi kama alijua kifo chake, jana (juzi) nilipokwenda kwake kumpa taarifa za kuitwa timu ya taifa alifurahi sana, aliweka muziki na kufungulia kwa sauti kubwa huku akicheza.
Nakumbuka kabla ya mechi yetu na Simba alinipigia simu akiniomba nimwekee jezi yangu ili tubadilishane kama kumbukumbu kwake,” alisema Niyonzima.

Saa 3:06 asubuhi

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa aliwasili Muhimbili, alianza kumwaga machozi huku akiwa amemkumbatia Uhuru Selemani.
Akizungumzia msiba huo, Pawasa alisema: “Nimeumia sana kusikia kifo cha Mafisango, mimi ndiye niliyemleta marehemu Azam FC kabla ya kujiunga na Simba, nilijuana naye nikiwa naichezea APR na niliishi naye chumba kimoja tukiwa na Laurent Kabanda ‘Mkandala’ ambaye naye amefariki, hivi sasa nimebaki peke yangu.”

Saa 3:41 asubuhi
Wanamuziki wa Akudo Impact wakiongozwa na Christian Bella, Cannal Top, Boteku Clary ambapo walisema kuwa walikuwa na marehemu kwenye Ukumbi wa Maisha dakika chache kabla ya kifo chake.
Akielezea kilichotokea muda mfupi kabla ya umauti wa Mafisango, mpiga drum wa Akudo, Boteku alisema baada ya FM Academia kumaliza kutumbuiza, Mafisango na wenzake walitoka ukumbini hapo wakiwa na wanawake wawili.
“Kabla ya kuondoka Mafisango alitoa shilingi elfu tano na kumpa Cannal Top na kumuambia aendelee kupata kinywaji halafu wakaondoka. Lakini awali hakuwa akitaka kuondoka,” alisema Boteku.

Mazishi:
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema kuwa mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi na utaagwa leo Ijumaa saa nne asubuhi katika Uwanja wa TCC Chang’ombe jijini Dar, kisha utasafirishwa kesho Jumamosi kwenda DR Congo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
“Familia yake ndiyo ambayo imeamua mwili upelekwe DR Congo, wao ndiyo watakaotoa uamuzi juu ya siku rasmi ya maziko, kama iwe Jumamosi au Jumapili. Kwa sasa kinachofanyika ni kushughulikia masuala ya pasi za kusafiria,” alisema Kaburu.
Kiungo huyo nyota wa Simba wakati wa uhai wake, ameacha mke, Rosina na watoto watatu Devictable (7), Crespo (5) na Patrina, mwenye mwaka mmoja.

Stori:
Wilbert Molandi na Khatimu Naheka