POLISI mkoani Tanga wamemuua kwa kumpiga risasi mtu anayedhaniwa kuwa ni jambazi akiwa katika harakati za kutoroka .

Mtu huyo alikuwa anatuhumiwa kuiba fedha kwenye duka la mfanyabiashara Soud Seif wa kijiji cha Mhinduro , Wilaya ya Mkinga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Costantine Massawe amemtaja mtu huyo kuwa ni Mlekwa Kwanyenye (45) ambaye ni mkazi wa Makorora mjini Tanga.

Amedai kuwa, Kwanyenye ni jambazi sugu na aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kufanikiwa kuiba fedha kutoka kwenye duka la mfanyabiashara maarufu katika kijiji hicho cha Mhinduro, kata ya Daluni wilayani humo.

Kwanyenye inadaiwa alitoka gerezani miezi mitatu iliyopita baada ya kumaliza kifungo chake katika Gereza la Maweni mjini hapa kwa kosa la ujambazi.

Duka lililoibiwa ni la mfanyabiashara anayejishughulisha na kazi ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya mtandao wa simu za mkononi.  

Massawe alisema mpaka sasa thamani ya fedha zinazodaiwa kuchukuliwa bado haijafahamika ingawa mmiliki anadai kwamba ni mamilioni ya Shilingi.

Alidai kuwa polisi ilipata taarifa kutoka kwa mmiliki wa duka hilo aliyepiga simu katika Kituo cha Polisi cha Mhinduro na wakati askari wakikaribia katika eneo la tukio, walisikia milio ya risasi ikilia hewani.

Kamanda Massawe alidai askari walimkimbiza Kwanyenye hadi katika mabonde huku wakijibizana risasi na katika piga nikupige alipigwa risasi ya tumboni na kufa papo hapo.

Mwili wake ulihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo na kwamba polisi wanaendelea kufanya uchunguzi kubaini kama kuna watu waliokula njama na mtuhumiwa huyo.

Wakati huohuo, Thomas Dominick anaripoti kutoka Musoma kuwa, mkazi wa kijiji cha Katario, tarafa ya Makongoro, Musoma vijijini, Duke Mkama (27) amepigwa risasi mguu wa kulia akijaribu kuwakimbia askari waliokwenda kumkamata.

Mtuhumiwa huyo anayedaiwa kuwa jambazi. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robert Boaz alidai kuwa Mkama alipigwa risasi Mei 9 mwaka huu.

Amedai kuwa Mkama anatuhumiwa kushiriki katika matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha na alikuwa anatafutwa siku nyingi.

Kamanda Boaz alisema kuwa mtuhumiwa huyo kwa sasa yupo katika Hospitali ya Mkoa akiuguza majeraha na atakapopata nafuu atahojiwa na kufikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.