Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amewasili mjini Khartoum katika jitihada za kufufua mazungumzo kati ya Sudan na jirani zao Sudan kusini.
Mpatanishi huyo wa Umoja wa Afrika anatarajiwa kukutana na Rais wa Sudan Omar al-Bashir. Lengo la mkutano wao ni kubuni ajenda na ratiba ya gumzo kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Mapigano makali kati ya Sudan Kusini na jirani zao Sudan mwezi uliopita karibu utumbukize mataifa hayo jirani katika vita .

Shirika la Umoja wa Mataifa limetishia kuziwekea nchi hizo mbili vikwazo.
Kulingana na kamati ya usalama ya Umoja wa Mataifa , nchi hizo mbili zilipaswa kuanza gumzo kati yao wiki iliyopita.

Sudan kusini kwa upande wake inasema iko tayari kurudi katika meza ya mazungumzo bila ya masharti yeyote. Lakini Sudan kwa upande wake inasisitiza kuwa gumzo kati yao lazima lijikite katika swala la usalama.