Richard Bukos na Imelda Mtema
UWANJA wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, juzi Jumapili, uligubikwa na vilio kila kona wakati ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa filamu walipokuwa wakimuaga staa wa tasnia hiyo Bongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ aliyekuwa akisafiri kwenda nchini India kwa matibabu, Risasi Mchanganyiko lina kila kitu.
Sajuki ni mgonjwa kwa muda mrefu sasa, alikwama kuendelea na matibabu kutokana na kukosa fedha, lakini baada ya michango ya Watanzania, amefanikiwa kupata fedha na siku hiyo ndiyo alikuwa akisafiri kwenda nchini humo katika Hospitali ya Apollo kutibiwa.
Juma Kilowoko ‘Sajuki’ akiagwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea nchini India.
HUZUNI KILA KONA
Tangu mishale ya saa nane na dakika kadhaa mchana, wasanii na wadau mbalimbali wa filamu walikuwa wameshaanza kuingia katika uwanja huo kwa lengo la kuagana na Sajuki.
Wengi walionekana kuwa na huzuni kubwa, huku wengine wakisikika wakimuombea dua, Mwenyezi Mungu amuepushe na majaribu hayo.
Saa 8:47 mchana, gari alilopanda Sajuki, mkewe Wastara Juma, mama mzazi wa Sajuki, Zaituni Mzena na ndugu wengine wa karibu liliingia uwanjani hapo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baada ya kuona gari hilo wasindikizaji walianza kuonekana kulengwalengwa na machozi, ndipo mmoja wa ndugu zake, alimfungulia mlango na kumshusha Sajuki.
AJARIBU KUSIMAMA, ASHINDWA
Mara baada ya Sajuki kushushwa kwenye gari, moja kwa moja alipokelewa na mhudumu wa ndege aliyekuwa na kiti maalum cha kubebea wagonjwa ‘wheel chair’.
Katika kuwapa moyo, ndugu jamaa na marafiki, Sajuki alitaka kujitahidi kusimama mwenyewe ili atembee, lakini alishindwa, hali hiyo ilizidisha simanzi na hapo ‘wenye mioyo midogo’ walianza kumwaga machozi.
Msanii Wastara ambaye ni mke wa Sajuki nae akitokwa na machozi.
ASHINDWA KUZUNGUMZA
Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliokuwa uwanjani hapo, walimfuata Sajuki wakati akisukumwa na kiti chake na kutaka kuhojiana naye kabla ya safari hiyo, lakini ilishindikana.
Sajuki, alipoona waandishi ambao wengine walikuwa na vipaza sauti, alifungua kinywa chake na kujaribu kuzungumza, lakini ghafla alishindwa kusema chochote na kubaki kimya.
Hilo liliwahuzunisha wadau waliokuwa uwanjani hapo, mmoja akashauri aachwe kwa kuwa hali yake haikuwa nzuri.
Kwa kumtazama Sajuki, pamoja na kwamba hakuweza kuzungumza lakini sura yake ilionesha wazi matumaini ya kurejea nchini akiwa na afya njema; Ni kama alikuwa akisema: “Msilie wala kuhuzunika sana, Mungu akipenda nitarejea na kuungana nanyi tena.”
Dada zake Sajuki wakilia wakati wa kumuaga kaka yao.
ASHINDWA KUPUNGA MKONO
Baada ya kugundua kuwa hakuwa na nguvu ya kuzungumza, Sajuki aliamua kuinua mkono wake ili kuwapungia wadau lakini zoezi hilo pia kwake lilikuwa mzigo.
Alionekana kuinua mkono wake kwa tabu kubwa, lakini juhudi zake ziliishia begani na kushindwa hata kuuzungusha kiganja kama ishara ya kupungia kwa watu waliokuwa uwanjani hapo.
Jambo hilo lilikuwa sawa na msumari wenye moto kwa wadau waliokuwa uwanjani hapo, ambapo walizidisha vilio kila kona.
Mama mzazi wa Sajuki, Bi. Zaituni akiwashukuru Watanzania kwa michango yao iliyofanikisha safari ya mwanae kwenda nchini India.
Mhudumu wa uwanjani hapo, aliyekuwa akimsukuma Sajuki, alishangazwa na namna umati wa watu ulivyojitokeza kwa wingi kwa lengo la kuagana na rafiki yao kipenzi.
Wakati watu waliokuwa uwanjani hapo wakiendelea kumpungia, Sajuki aliingizwa moja kwa moja katika chumba cha abiria wanaoondoka na kumuacha Wastara nje.
WASTARA AACHA KICHANGA KIKILIA
Katika hali iliyozidisha uchungu kwa mashabiki wa Sajuki waliokuwa uwanjani hapo, Wastara alilazimika kumuacha mwanaye mchanga kwa wifi yake (dada wa Sajuki) aitwaye Naima Kilowoko.
Ilielezwa kuwa, Wastara alilazimika kumuacha mwanaye kwa wifiye kwa sababu nyingi, ikiwemo kuwa huru kwa ajili ya kumhudumia mumewe kwa karibu muda wote wakiwa hospitalini.
Wakati mtoto huyo akikabidhiwa kwa shangazi yake, aliangulia kilio kikali, kama vile alikuwa akijua kwamba wazazi wake wapo kwenye matatizo.
“Mh! Kweli watoto ni Malaika, maskini inawezekana halii kwa sababu anaachwa, bali naye ameona kwamba baba yake ni mgonjwa,” alisikika mmoja wa wadau akisema.
Wastara alipokuwa akimpa wifi yake mtoto, alisikika akimwambia maneno ya uchungu: “Wifi tunakuachia mwanetu, tunaomba umuangalie vizuri, nafikiri unaona matatizo yetu. Sisi siku ya kurudi haijulikani, tuendelee kuombeana dua.”
Hali ilikuwa mbaya zaidi, Wastara aliposema maneno hayo huku akilia, wakakumbatiana wakizidi kulia pamoja na mtoto.
Wakiwa katika hali hiyo, mama mzazi wa Sajuki, Zaituni ambaye alikuwa akilia karibu wakati wote uwanjani hapo, naye aliungana nao na kuzidisha uchungu kwa watu wengine waliowashuhudia.
MAMA AWASHUKURU WATANZANIA
Baada ya Wastara kuingia katika chumba cha abiria wanaoondoka kumfuata mumewe, mama mzazi wa Sajuki, Zaituni alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watanzania wote waliochangia kuokoa maisha ya mwanaye.
“Siwezi kusema chochote, Mungu ndiye anayejua ni kwa namna gani ninawashukuru kwa moyo wenu wa upendo. Nawaombea dua wote waliojitoa kwa hali na mali kwa ajili ya mwanangu. Mungu atawarudishia.
“Kipekee naomba niwashukuru rais wetu, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wabunge na wengine wote waliochangia. Nasema ahsanteni sana na Mungu atawalipa,” alisema kwa uchungu bi. Zaituni.
BAADHI YA WASANII WALIOHUDHURIA
Wasanii waliofika kumuga Sajuki ni pamoja na Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’, Nuru Nassor ‘Nora’, Sabrina Rupia ‘Cathy’, Mohammed Mwikongi ‘Frank’ na wengine wengi.
KALAMU YA MHARIRI
Umoja waliouonesha Watanzania kwa maradhi ya Sajuki ni mkubwa na unaopaswa kupongezwa. Huu ndiyo upendo wa kweli tunaopaswa kuwa nao.
Tunawaomba ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi wa Sajuki watulie na kuondoa mashaka mioyoni mwao, maana Mungu mwenye nguvu anaweza kumsaidia ndugu yetu na kurejea nchini akiwa mwenye afya.
Dua zetu Watanzania, kwa sasa ndiyo kitu muhimu zaidi kwa Sajuki na familia yake.
0 Comments