Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki kuimba wimbo wa wafanyakazi akiwa kashikana mikono na Rais wa Jumuiya ya Vyama vya wafanyakazi (TUCTA), Omary Ayub Juma, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa kwenye sherehe za Mei Mosi katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. (Picha na Ikulu).


RAIS Jakaya Kikwete amefurahishwa, tena hana kinyongo na mjadala wa ubadhirifu wa fedha za umma ulioibuliwa bungeni kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati za Fedha za Bunge na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo mapema iwezekanavyo.

Ripoti hiyo ya 2009/2010 iliyowasilishwa katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 10 uliomalizika hivi karibuni, iligusa baadhi ya mawaziri ambao walidaiwa kuhusika na vitendo vya wizi na ubadhirifu wa fedha za umma ambapo wabunge walipendekeza mawaziri hao wajiuzulu.

Pamoja na suala la ubadhirifu, Rais Kikwete pia amewaahidi wafanyakazi nchini kuboreshewa mazingira yao ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuongezwa mshahara kila mwaka na mwaka huu, Sh trilioni 3.2 kati ya Sh trilioni 6.7 zitatumika kwa mishahara.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa Tanga jana na kutangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari, Rais Kikwete alisema kuibuka kwa mjadala huo ni matokeo ya kazi yake nzuri ya kusisitiza uwazi katika ripoti hizo za CAG tofauti na miaka ya nyuma.
“Taarifa ya CAG ya mwaka 2009/2010 iliwasilishwa na kujadiliwa, huku kukiwa na mapendekezo mbalimbali kutoka bungeni na umma kwa jumla, wengine wakitoa rai mawaziri wawajibishwe…nawahakikishia sijakasirishwa wala kukarahishwa na mjadala huo, nimefurahi kuwa taarifa hii imepewa uzito unaostahili,” alisema Rais Kikwete.

Alichokuwa akikitaka Alisema kilichotokea bungeni ndicho alichokuwa akikitaka na amefurahi kuona yakitekelezwa ambapo alibainisha kuwa amejipanga vema kuhakikisha mapendekezo yote yanatekelezwa.

Alisema tangu aingie madarakani mwaka 2005 alipendekeza taarifa zote za uchunguzi kuhusu utendaji wake ziwekwe wazi.

“Mimi naamini katika mambo ya uwazi, nataka mambo yote yanayokaguliwa wananchi wayajue, mnayaficha mnaogopa nini?



Alisema kabla ya hapo, taarifa za ukaguzi wa Serikali zilikuwa hazisikiki na hata zikikamilika, mjadala wake haukuwa wa wazi wala mapendekezo yalikuwa hayafanyiwi kazi na hata bungeni zilikuwa hazisomwi zaidi ya kuwasilishwa mezani.

“Kabla ya kuwa Rais, wakati wa kampeni nililisemea sana suala la nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali, nilikuwa natumia sana neno mchwa, kwamba kwenye halmashauri jamani kuna mchwa tena mchwa hao ni hatari wanakula mpaka noti,” alisema.

Alisema hata baada ya kuwa Rais, alisisitiza juu ya nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali na katika moja ya mikakati yake ya kufanikisha hilo, aliimarisha kwanza ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, kwa kuwa hicho ndicho chombo cha kuishauri Serikali na Septemba mwaka 2009 aliteua rasmi CAG. 
Alisema lengo lake ni kutaka usimamizi wa fedha za umma na zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa, badala ya kunenepesha matumbo ya baadhi ya viongozi wasio waadilifu na hadi sasa amefanya vizuri kiasi cha kuwakasirisha baadhi ya viongozi.

“Yule bwana yuko pale kwa mujibu wa sheria, hakuna chombo chochote nchini chenye mamlaka ya kuondoa au kusema adhibitiwe, kwa kuwa amefichua yasiyotakiwa, kama mtu hakuridhika na kilichofichuliwa aende mahakamani,” alisisitiza.

Alisema ripoti ya kwanza ya CAG ilimfadhaisha na kumtisha kutokana na kugundua ubadhirifu mkubwa katika matumizi ya fedha za Serikali, kiasi cha kumfanya Rais aitishe Baraza la Mawaziri na makatibu wakuu na kumwita CAG, Ludovick Utouh aelezee uozo aliobaini na juzi aliitisha mkutano wa viongozi wa halmashauri za wilaya ambao pia walikutana na Utouh.

Ajira na wafanyakazi Awali akizungumzia suala la ajira na wafanyakazi, alisema Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa inaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya wafanyakazi kwa kuongeza mishahara yao kila mwaka na pia kudhibiti mfumuko wa bei ambao umekuwa mzigo kwa wafanyakazi.

Aidha, aliahidi kufanyia kazi suala la kupunguza kodi ya mapato na kupunguza misamaha ya kodi na kupanua wigo wa walipa kodi kama vile wakulima, wafugaji na sekta nyingine ambazo hadi sasa hazijaingizwa kwenye mfumo wa kodi, ili kuongeza mapato ya Serikali.

Alihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki sensa ya watu inayotarajiwa kufanyika Agosti 26 na kutoa maoni yao kwa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba iliyoanza kazi rasmi jana.
Alihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki sensa ya watu inayotarajiwa kufanyika Agosti 26 na kutoa maoni yao kwa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba iliyoanza kazi rasmi jana.

Maombi ya wafanyakazi Mapema akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Nicholas Mgaya alisema kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Mishahara duni, kodi kubwa na mfumuko wa bei ni pigo kwa wafanyakazi’.

Alisema kutokana na kaulimbiu hiyo, wanamwomba Rais awezeshe nyongeza ya mishahara ya kima cha chini na kufikia Sh 315,000 kwa mwezi, kupunguza makato ya kodi ya mapato, kusimamia ipasavyo maslahi ya wastaafu, kufanyia kazi matatizo sehemu za kazi na kuwawajibisha mawaziri wote waliohusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Mawaziri wanaotuhumiwa katika kashfa mbalimbali ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu. Mawaziri wengine wanaohusishwa na ubadhirifu huo ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk Jumanne Maghembe; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.