Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wakiwa kwenye maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, yamefanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Eugen Mikongoti (aliyevaa koti jeusi), akiongoza maandamano ya wafanyakazi wa mfuko huo, kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja,Jijini Dar es Salaam
Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wakiwa na furaha wakati wa maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, yamefanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.Ni furaha kwa kila mfanyakazi wa mfuko huo.
Na Grace Michael
WAFANYAKAZI wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wameahidi kufanya kazi kwa kujituma ili kuhakikisha kauli mbiu ya Mfuko huo ya “Miaka kumi ya kuaminiwa na kujituma, Huduma bora za matibabu na Afya bora kwa wote” inatekelezwa kwa vitendo.
Ahadi hiyo waliitoa muda mfupi katika viwanja vya Mnazi Mmoja,Dar es Salaam, baada ya kumaliza maandamano ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Mfuko huo, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Eugen Mikongoti, alisema kuwa pamoja na changamoto chache zinazoukabili Mfuko huo kwa sasa lakini wafanyakazi wa Mfuko huo watafanya kazi kwa kujituma na kwa uaminifu mkubwa ili kuhakikisha wanachama wake wanapata huduma kwa heshima inayostahili.
“Sisi kama wafanyakazi wa NHIF, tunawaahidi wanachama wetu kuwa tunafanya kazi kwa uaminifu mkubwa na kwa kutanguliza maslahi yao ili hata wanapofika katika vituo vya kutolea huduma wapate huduma kwa heshima na hilo ndilo lengo letu kubwa, tunataka kauli mbiu yetu ionekane kwa vitendo,” alisema Mikongoti.
Kutokana na hayo, alisema kuwa wafanyakazi wa Mfuko huo wanaungana na wafanyakazi wengine duniani kote kuadhimisha sikukuu hiyo ambayo kama Mfuko wataitumia kama chachu ya kuongeza uwajibikaji.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE wa Tawi la Bima ya Afya, Baraka Maduhu, alisema kuwa pamoja na kauli mbiu ya wafanyakazi kitaifa kudai nyongeza ya mshahara, aliwataka wanachama wake kuhakikisha wanatimiza wajibu ili wanapodai haki zao waweze kueleweka.
“Haki na wajibu ni vitu pacha hivyo mfanyakazi ili aweze kueleweka ni lazima anapodai haki zake ahakikishe naye ametimiza wajibu wake ipasavyo, mimi kama kiongozi wao, naahidi kutetea maslahi yao muda wote na lengo kubwa ni kuhakikisha huduma kwa wanachama wetu zinakuwa bora zaidi,” alisema Baraka.
Naye Mwenyekiti wa Wanawake NHIF, Fortunatha Raymond, alisema kuwa akiwa kama kiongozi mwanamke atatumia fursa aliyonayo kuhakikisha wafanyakazi wa NHIF hasa wanawake wanakuwa kinara katika utendaji kazi wao na kuondokana na dhana ya utegemezi.
Baada ya maadhimisho hayo, wafanyakazi hao walitumia fursa hiyo kukutana pamoja na kubadilishalishana mawazo lakini kubwa ni kupeana mikakati ya namna ya kuwatumikia wanachama wao.
0 Comments