SERIKALI imepiga marufuku taasisi binafsi zilizokuwa zikikopesha walimu bila kufuata taratibu zinazotakiwa na kuanzia sasa watakaoruhusiwa ni wale watakaokuwa na kibali kutoka kwa makatibu tawala wa mikoa baada ya kubainika kuwa walimu wengi hawahudhurii vipindi kutokana na kukimbia wanaowadai.
Tamko hilo lilitolewa juzi na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa wakati wa kufunga kikao kazi cha siku tatu kilichoshirikisha makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi watendaji wa Halmashauri na wataalamu wa fedha wa mamlaka za Serikali za Mitaa.
Majaliwa alisema walimu wengi hawaingii madarasani kwa kukimbia waliowakopesha, hali inayochangia mahudhurio yao katika vituo vya kazi kuwa mabaya kutokana na kutumia muda mwingi kuhangaikia mikopo.
Alisema wakati mwingine walimu hukosekana kwenye vituo vya kazi kwa zaidi ya siku tatu wakihangaika wakitafuta fedha za kulipa madeni.“Ni marufuku taasisi yoyote kuhamasisha na kushauri walimu wakope au kwenda mashuleni kwa lengo la kushashawishi walimu kukopa katika taasisi zao. Mikopo yote ambayo inatakiwa kutolewa kwa walimu lazima iwe na kibali kutoka kwa Katibu Tawala,” aliagiza Naibu Waziri.
Alisema katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili walimu, kila halmashauri inatakiwa kuhakikisha kuwa inatambua matatizo ya walimu na kuyatafutia ufumbuzi mapema na si kusubiri mpaka matatizo kuwa mengi na kushindwa kuchukua hatua yoyote.
“Cha kushangaza utasikia mtumishi aliyeajiriwa tangu 2008 hana mshahara tangu Januari mwaka huu, wakati siku za nyuma alikuwa akipata mshahara kama kawaida, ukiuliza kwa nini inakuwa hivyo wakati mtu tayari aliingizwa kwenye utaratibu wa kuingiziwa mshahara utaambiwa kuna tatizo.
Lipo eneo tunalokosea na wakati mwingine ukosefu wa mawasiliano,” alieleza Naibu Waziri. Naibu Waziri alisema suala la watumishi wapya lipewe kipaumbele kwa kuhakikisha wanaripoti kwa wakati kwenye vituo vyao vya kazi na madai yao ya kuingizwa kwenye orodha ya kupatiwa mishahara mara moja na si kusubiri muda upite na kuanza kushughulikia masuala yao baada ya kuanza kupata malalamiko.
Aidha, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaboresha miundombinu, ikiwamo kukarabati shule zote kongwe ili kurudisha hadhi ya shule hizo.
Alisema vitabu milioni mbili vya sayansi vilisambazwa nchi nzima na lengo ni kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anakuwa na kitabu cha kila somo. Katika hatua nyingine, wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini na makatibu tawala wa mikoa wametakiwa kwenda kujipanga upya katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha hakuna halmashauri itakayokuwa na hati chafu ambazo huchangiwa na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia aliyasema hayo wakati wa kufunga kikao kazi cha siku tatu kilichoshirikisha makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi watendaji wa halmashauri na wataalamu wa fedha wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu matokeo ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2010/2011.
Ghasia alisema kila mkurugenzi na katibu tawala ahakikishe kuwa nakala ya hotuba aliyoitoa wakati wa kufungua mkutano huo inawafikia wakuu wote wa Idara, kufanya nao vikao, kujadili waliyokubaliana ili kuhakikisha hati chafu na zenye mashaka hazitakuwapo.
Aidha, aliwataka wakajibu hoja zote za wakaguzi ambazo hazijajibiwa na majibu hayo yapitishwe kwenye ngazi za kisheria kisha kupitia kwa Mkuu wa Mkoa na hatimaye majibu hayo yafike kwenye Ofisi ya CAG na baadaye watakutana kwenye kikao cha kujadili majibu ya hoja hizo kwenye kikao kitakachoitishwa baadaye.
Alisema waliohusika na ubadhirifu na hoja zao ambazo hazijajibiwa ambao walikuwa wakitoa sababu mbalimbali kama kupotea kwa vitabu vya risiti, wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
“Kila mmoja awajibike kutekeleza mpango tuliojiwekea…sisi ni watu wazima tumekubaliana kila mtu aende kutimiza wajibu wake,” alisema Ghasia na kutaka fedha zinazotolewa na Serikali kuhudumia wananchi, zitumike kwa matarajio yaliyokusudiwa ikiwamo kuwa na takwimu sahihi za watumishi katika halmashauri kwani kuna mishahara hewa mingi inaendelea kulipwa kwa watu ambao hawako kwenye utumishi.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Hussein Katanga alisema anaamini kutokana na kikao kazi hicho kutakuwa na mabadiliko ya kiutendaji na kuwataka kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu yao. Pia aliwataka kuacha kuwapa mafunzo watumishi wanaokaribia muda wa kustaafu.
0 Comments