Na Haruni Sanchawa RAIA mmoja wa Bulgaria, Petez Ninkov, 32, (pichani) amenusurika kuuawa baada ya kudaiwa kuiba fedha katika mashine ya kuchukulia fedha (ATM) jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika Benki ya Standard Chartered, Tawi la Ilala ambapo mzungu huyo aliponea chupuchupu kupigwa baada ya kuokolewa na polisi ambao walikuwa doria na haraka wakamkimbiza polisi.
Habari ambazo tumezipata zinaeleza kuwa, tayari amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu mashitaka ya kuiibia benki hiyo fedha taslimu shilingi milioni 35.
Ninkov amefikishwa katika mahakama hiyo kujibu shitaka hilo la wizi katika benki hiyo tawi la Ilala jijini Dar es Salaam.
Mwendesha mashitaka wa serikali, Aidah Kisumo alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Februari 6 na Aprili 4 mwaka huu.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, kati ya siku hizo mtuhumiwa aliiba Dola za Kimarekani 23,000 kutoka katika mashine ya kuchukulia fedha (ATM), mali ya Benki ya Standard Chatered huku akijua kuwa ni kosa.
Katika shitaka la pili Mwendesha mashitaka alidai kuwa, mtuhumiwa aliiba tena Mei 17, mwaka huu katika benki hiyo baada ya kupanga njama ya kutenda kosa hilo.

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Tarsila Kisoka aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 6, mwaka huu na mshitakiwa ametupwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wanaotambuliwa na serikali ambao watasaini nusu ya mali iliyoibiwa.
Akizungumzia tukio hilo jana kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema ni lazima benki kuwa waangalifu kwa kuwa mbinu zinazotumika kwa wizi huo ni za kisasa. Ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa polisi wakimtilia shaka mtu yeyote aliye katika mashine za ATM
.