Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha- Rose Migiro akiwa na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Watanzania waishio Jijini New York na vitongoji vyake.
Naibu Katibu Mkuu, akiwa na timu ya viongozi waliomtembelea ofisi kwake akiwamo pia Kaibu Balozi, Justin Seruhere na Balozi Tuvako Manongi muda mfupi kabla ya kufanya mazungumzo na kubadilishana mawazo na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania.
                    Hapa Naibu Katibu Mkuu akiwa na wajumbe wa Bodi ya wadhamini.

Na Mwandishi Maalum

Watanzania waishio ughaibuni wameshauriwa kushiriki kikamilifu kwa kutoa mawazo, mapendekezo na maoni yao kuhusu mchakato wa maandalizi ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania.

Ushauri huo umetolewa siku ya Alhamisi na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Watanzania waishio Jijini New York na Vitongoji vyake.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake, Migiro amesema kwamba, kama ilivyo kwa watanzania wengine, watanzania waishio nje ya Tanzania nao wanawajibika kujikusanya na kujipanga na kutoa maoni yao, ushauri na mapendekeo kwa Tume ya Katiba ya nini wadhani kinafaa kuingizwa katika katiba Mpya.

“ Mkijipanga vizuri mnaweza kabisa kuchangia mijadala ya kuundwa kwa Katiba Mpya. Na mnaweza kufanya hivyo kwa kutumia vyombo mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii, ( Social media) na sauti zenu zikasikika ili mradi mjipange vizuri” akasema Migiro.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Kaibu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt. Justin Seruhere na Balozi Tuvako Manongi kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Naibu Katibu Mkuu.

Aidha Naibu Katibu Mkuu, licha ya kuwahimiza watanzania waishio nje ya nchi kushiriki katika mijadala ya maandalizi ya Katiba mpya. Amewataka pia watanzania waishio jijini New York na vitongoji vyake, kuendelea kushirikiana, kusaidiana na kushikamana kupita Jumuiya yao.

Akasema ni kwa kupitia jumuiya hizo, ndipo wanapoweza kubadilishana mawazo, kupashana habari ya nini kinachoendelea nchini mwao, lakini kubwa zaidi ni kusaidia kule walikotoka.

Akasema kwamba ni kwa kutambua umuhimu wa watanzania waishio nje ya nchi na mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ndiyo maana Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kushirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa , Mhe. Bernard Membe imeundwa Idara maalum ya Diaspora.

Akafafanua kwamba zipo nchi ambazo uchumi wake unaendeshwa na michango inayotoka kwa wananchi wao waishio na kuendesha shughuli zao nje ya nchi zao.

“ Hata ninyi mnaweza kabisa kuwa chachu na kichocheo kikubwa cha ukuzaji wa uchumi wa nchi yetu Tanzania, kuwasaidia ndugu zenu mliowaacha nyumbani lakini pia mkaanzisha miradi ya kijamii. Haya yote yanawezakana kama tu mtakuwa kitu kimoja na kushirikiana kwa karibu na hasa ikizingatiwa kwamba kwa mila na utamaduni wetu watanzania ni watu wakushirikiana”. Akasisitiza Migiro.

Akatumia nafasi hiyo kuwashukuru watanzania wote waishio jijini New York na vitongoji vyake, kwa namna walivyompokea na kushirikiana naye kwa karibu katika kipindi chote cha miaka mitano na nusu cha Unaibu Katibu Mkuu.

Akasema kwa dua zao, upendo wao na ushirikiano wao vimechangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yake, majukumu ambayo amesema yalikuwa na changamoto nyingi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya watanzania waishio New York na Vitongoji vyeke, Bw. Hajji alimweleza Naibu katibu Mkuu kwamba watanzania wamefurahishwa na kuridhishwa sana na namna alivyoibeba na kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika Umoja wa Mataifa tangu mwazo wa wadhifa wake hadi dakika ya mwisho.

Akasema kwamba, hapana shaka kila mtanzania amekuwa kitembea kifua mbele kwa uwepo wake katika wadhifa huo mkubwa na kwamba wanamtakia kila la kheri na mafanikio makubwa pindi akirudi nyumbani. Na wataendelea kujivunia utumishi wake uliotukuka.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha- Rose Migiro anatarajiwa kumaliza majukumu yake mwishoni mwa wezi huu wa Juni.