Na Saleh Ally
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo amekubali kuifundisha Yanga na imeelezwa usajili wa beki Kelvin Yondani ni msisitizo wake kabla hajatua nchini.
Hivi karibuni mbele ya Rais Jakaya Kikwete alipokuwa ziarani nchini Brazil, Maximo alisema hatarejea kuifundisha timu ya taifa na alikuwa akiendelea kufanya kazi katika klabu yake ya Democrata-GV ya Brazil.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinaendelea, Maximo amekubali kwa asilimia 100 kuifundisha Yanga na ameutaka uongozi wa klabu hiyo kufanya makubaliano na klabu yake, iwapo atakubali, basi ataanza rasmi kazi ya kuinoa klabu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Kagame, au baada ya hapo.
“Maximo amekubaliana na Yanga kwa kila kitu, suala la mshahara halina tatizo kwa kuwa hauna tofauti na ule aliokuwa analipwa Kosta Papic. Hivyo Yanga imekubali kumlipa na akifika tu atapewa mishahara ya miezi mitatu kabisa.
“Pamoja na vitu vyote, Maximo ameomba kuja na msaidizi wake ambaye atafanya naye kazi pamoja na kila kitu kimekubaliwa. Hivyo klabu yake imekubali, atakuja na msaidizi wake katika timu hiyo anayoifundisha na mazungumzo yanahusisha watu wote hao wawili.

“Kingine atakachopewa ni gari nzuri ya kutembelea pamoja na nyumba katika eneo la Masaki, Mikocheni au Msasani na kila kitu kipo tayari,” kilieleza chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga. Mazungumzo kati ya klabu ya Maximo na Yanga yameshaanza na inaonekana huenda mambo yakaenda vizuri na kocha huyo akarejea nchini, safari hii akiwa katika ngazi ya klabu.
Katika mkataba wake wa mwanzo akiwa na Taifa Stars, Maximo alikuwa analipwa dola 10,000 (zaidi ya Sh milioni 16) na alipongia mkataba wa mwisho akaanza kulipwa dola 15,000 (zaidi ya Sh milioni 24).
Yanga ambayo inaendelea kusajili kikosi imara chini ya usimamizi wa Yusuf Manji unaoongozwa na kamanda wa jeshi lake, Seif Mohammed ‘Magari na Ahmed Bin Kleb, imeamua kupata kocha wa uhakika ingawa kuna maombi zaidi ya makocha 20 ambao wameomba kuinoa.
Kabla ya kuondoka Maximo alimteua Yondan katika kikosi cha Stars na kumchezesha pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, pia alisema Yondani ameiva kuichezea Stars.
Wakati anajiandaa kuiachia Taifa Stars, Maximo alikuwa anawindwa na klabu mbili, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na nyingine kutoka nchini Israel lakini mwisho aliamua kurejea kwao Brazil na kuendelea na kazi ya kufundisha.