Na Mwandishi wetu
HEKAHEKA ya wimbi la mastaa wa Bongo kutumika kwenye imani inayodaiwa kuwa ni ya kishetani duniani maarufu kwa jina la Freemason a.k.a Wajenzi Huru inazidi kuchukua nafasi kwa kasi baada ya hivi karibuni kudaiwa kuwa, staa wa sinema za Bongo, Jacqueline Wolper Massawe naye ametumbukia humo, Risasi Jumamosi limesheheni.
NI NCHINI AFRIKA KUSINI
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, Wolper ameinamisha kichwa na kumwagiwa maji ya imani hiyo kama ishara ya kujiunga nchini Afrika Kusini, mapema mwaka huu.
NANI SHAHIDI?
Mmoja wa marafiki wa Wolper aliliambia gazeti hili kwamba, Wolper alishawishiwa na msanii mwingine wa kiume wa filamu Bongo ambaye hana jina kubwa kuwa ndiye aliyempa namba za mawasiliano za wahusika nchini Afrika Kusini.
“Wolper ameingia Freemason na aliyemshawishi ni msanii ….(anataja jina), yeye alimwambia akiwa huko anaona matunda yake kwani ni imani ambayo binadamu unaishi kama peponi,” alisema rafiki huyo.
UTAJIRI WA HARAKA WATAJWA
Kwa mujibu wa chanzo hicho, tangu Wolper amejiunga na imani hiyo inayosambaa kwa kasi nchini Tanzania amekuwa akipata mafanikio makubwa tena kwa haraka.
“Wee kama unataka kuamini, angalia tangu mwaka huu (2012) umeanza, Wolper mambo yanamyookea tu. Awali alikuwa akiishi eneo ambalo halimfai kama staa, sasa amehamia Mbezi, tena kwenye jumba zuri sana,” alisema mtoa habari huyo.
Aliendelea kuweka wazi kuwa, magari na miradi mingine aliyonayo si ofa kutoka kwa mchumba wake aitwaye Abdallah Mtoro ‘Dallas’ kama anavyodai mwenyewe Wolper bali ni ‘baraka’ ya Freemason.
Akasema: “Mmekuwa mkiandika eti kanunuliwa magari na mchumba wake, nani kasema? Ile ni kama njia ya kukwepea tu, lakini ukweli ni kwamba Freemason ndiyo wanambeba kwa sasa.”


Akaongeza: “Wazazi wa Wolper wapo katika wakati mgumu, mama yake amepata fununu za mwanaye kujiunga na Freemason na ndugu wakamweka chini kumwonya kama ni kweli ajitoe mara moja.”

KANUMBA ALIJIUNGIA NIGERIA
Hivi karibuni, mtu mmoja aliyejitaja kuwa ni mchungaji wa kanisa moja la kiroho jijini Dar, George Kariuki alizungumza kupitia Kituo cha Radio Times FM na kudai kuwa marehemu Steven Kanumba alijiunga na u-Freemason nchini Nigeria, nchi ambayo iko mbali kidogo kutoka Tanzania kuliko ilivyo Afrika Kusini anakodaiwa kwenda Wolper.
Hata hivyo, matokeo ya Kanumba kujiunga yalionekana, kupata mali kwa kasi ya ajabu, nyota yake kung’ara lakini mwisho wa yote ilifika mahali imani hiyo inatajwa na baadhi ya watu kuwa ndiyo chanzo kikuu cha kifo chake (Mungu amlaze pema peponi-amina).

BOFYA HAPA UMSIKIE WOLPER
Baada ya madai hayo, Risasi Jumamosi lilimsaka Wolper kwa nguvu zote na kubahatika kukutana naye siku ya Jumatano maeneo ya Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Baada ya salamu, msanii huyo mwenye aibu kwa mbali, alisomewa ‘mashitaka’ yake yote huku akiwa amemkazia macho paparazi.
Wolper: “Mh! jamani, mnajua haya mambo bwana yana siri kubwa ndani yake. Wako watu wanatajwa ni Freemason, wengine wapo lakini hawatajwi, ni kwa nini?”

WOLPER JIBU SWALI
Paparazi: “Labda kikubwa ungetuambia ni kweli upo huko au si kweli?”
Wolper: “Unajua bwana, mimi sina hela kama wanavyosema watu. Na haya yote yametokana na nilivyomsaidia Sajuki (Juma Kilowoko). Yule nilimsaidia kwa sababu niliguswa kutoka moyoni, lakini familia yangu yenyewe ina uhitaji mkubwa sana.
“Tena naomba jamii ielewe kuwa, sina ‘minoti’ ya kumwaga. Napata tabu watu wananifuata wakilia shida zao wakiamini nina fedha kibao, si kweli jamani.”

WOLPER VIPI?
Paparazi: “Umezungumza vizuri, lakini hujajibu suala la kujiunga na Freemason kama ni kweli au si kweli?”
Wolper: “Mimi gari si alininunulia Dallas, mbona nilishasema jamani au?”
Paparazi: “Sawa, ulishasema, vipi kuhusu Freemason sasa?”
Wolper: “Ni kwa sababu ya hizi nguo au? Maana nguo navaa bila kujua alama zake, sasa kama kuna za Freemason mimi nitajuaje jamani, ee?”

HAYA SASA
“Ila labda nikiri kitu kimoja, ni kweli niliwahi kuitwa na watu wakaniambia nijiunge kwenye imani hiyo, waliniahidi kwamba nikikubali maisha yangu yatakuwa mazuri na ulinzi wa afya yangu.”
Paparazi: “Ina maana hujajiunga unafikiria kwanza?”
Wolper: “We unaonaje, nijiunge au? Mimi sitaki nasikia wengi wameingia wanafanikiwa kwa kasi.”