Rais Jakaya Kikwete (katikati) akiongozana na Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh. Ally Hassan Mwinyi (awamu ya pili) na Mh. Benjamin Mkapa (awamu ya tatu) muda mfupi baada ya kumalizika kwa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia kuimarisha huduma ya afya kwa waathirika wa Virusi Vya Ukimwi (VVU), huduma za afya kwa ujumla hasa kwa kinamama wajawazito na watoto na kuimarisha mifumo ya taasisi katika sekta hiyo iliyofanywa na Taasisi ya Mkapa kupitia program yake ya Mkapa Fellows.
Rais Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa harambee hiyo iliyofanyika jana usiku kwenye ukumbi wa hoteli ya Hyatt Kilimanjaro,jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. Jakaya Kikwete akihutubia wakati wa harambee hiyo.
 Rais Mstaabu wa Awamu ya Tatu,Mh. Benjamin Mkapa akihutubia wakati wa harambee hiyo.

Kutoka kulia kwenda kushoto 1-3 ni wake wa marais wetu


Taasisi ya Mkapa imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 3.2 kupitia harambee ya mchango uliotolewa kwenye chakula cha hisani kwenye hoteli ya Kempinski, Jijini Dar es Salaam, Jumanne jioni (5/6/2012).
Kiwango hicho cha fedha kimepitiliza lengo lililokusudiwa na taasisi hii ambalo lilikuwa ni kukusanya shilingi bilioni 3 kupitia program ya Mkapa Fellows ambayo inalenga kuendesha miradi ya kusaidia huduma za afya nchini hasa maeneo ambayo huduma hizo ni hafifu. Huduma hizo zimejikita zaidi katika maeneo matatu; kuimarisha huduma kwa waathirika wa Virusi Vya Ukimwi (VVU), huduma za afya kwa ujumla hasa kwa kinamama wajawazito na watoto na kuimarisha mifumo ya taasisi katika sekta hiyo.
Fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo zilitolewa na watu mbalimbali baada ya kuhamasika na kuguswa na jinsi Taasisi ya Mkapa inavyowasaidia na kuokoa maisha ya Watanzania wengi hasa maneo ya vijijini.
Mgeni rami kwenye harambee hiyo alikuwa ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho ambaye alishirikiana na maraisi wastaafu, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na Benjamini William Mkapa.
Vitu mbalimbali vilinadiwa kwenye harambee hiyo zikiwepo picha za maraiasi hao walioingoza Tanzania kwa awamu tofauti tangu mwaka 1985.
Kabla ya kuanza mnada huo, tayari watu binafsi, mashirika na kampuni mbalimbali zilikuwa zimehamasika na kuchangia shilingi bilioni 1.5 ambazo zilikuwa ni nusu ya makadirio.
Mmoja wa wahamasishaji na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahamani Kinana amesema Mheshimiwa Mkapa amekuwa akishawishi wahisani wa nje waisaidie taasisi hiyo kufanikisha mikakati yake lakini safari hii ameona ni vyema Watanzania wenyewe wakachangia. Hali hiyo akaielezea itatia hamasa zaidi na kuonyesha moyo walio nao wananchi katika kuchangia maendeleo yake.
Ofisa Mtendaji wa Taasisi ya Mkapa, Dk Ellen Senkoro ametoa maelezo mafupi kuhusu taasisi hiyo, kazi inazofanya na kusudio la harambee.
Amesema kuwa mchango huo wa hisani wa shilingi bilioni 3 ni bajeti ya mwaka mmoja katika kutekeleza mpango wa miaka mitano wenye lengo la kuchangia jitihada za serikali kupambana na janga la Ukimwi, kuzuia vifo vya kinamama na watoto ili kutimiza malengo ya milenia namba nne, tano na sita. Mradi huo mzima utagharimi shilingi Bilioni 15.
Amesema Taasisi ya Mkapa tayari imejitanua na ina wanawafanyakazi waliosambaa nchi nzima jambo ambalo linampa moyo kuwa watafanikisha lengo walilokusudia kwenye kipindi hicho cha miaka mitano.
Mheshimiwa Rais Kikwete amekiri kwenye harambee hiyo kuwa pamoja na juhudi kubwa za serikali za kuimarisha huduma za afya nchini, bado huduma hizo hazijafikia kiwango kinachotakiwa kama inavyopendekezwa kitaalam.
Akaisifu Taasisi ya Mkapa kwa juhudi zake za kupunguza tatizo hilo huku akiwahamasisha watu mbalimbali waliohudhuria kuchangia ili kuleta matumaini kwa Watanzania, hasa waishio vijijini.
“Tunaihitaji sana Taasisi ya Mkapa na ufanikishaji wa miradi yake unategemea kujitoa kwenu katika kuichangia,” amesema Mheshimiwa Rais Kikwete.
Watu binafsi, mashirika, kampuni na taasisi mbalimbali zilishiriki kwenye chakula hicho cha hisani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Benjamini Mkapa kuendesha harambee kwa kuhamasisha Watanzania kuichangia.
Taasisi ya Makapa ni nini?
Taasisi ya Mkapa ni mfuko wa fedha wa kuendesha miradi ya afya kwa kuzingatia huduma kwa jamii bila kutegemea kuzalisha faida. Ilianzishwa Aprili 2006 kwa lengo la kusaidia juhudi za Serikali katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
Huu ni mradi ambao ulibuniwa na Watanzania kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania hasa wanawake, watoto na wa wale waishio na VVU.
Tayari Taasisi ya Mkapa imemaliza miradi ya awamu ya kwanza na sasa wanaanza ya pili. Inagwa walianza katika mikoa michache katika miaka mitano iliyopita tangu ilipoamzishwa mwaka 2006, tayari miradi yake imeenea nchi nzima.
                                                                     Kutoka kwa Issa M.Michuzi