Na Mwandishi Wetu
IMEKUWA utafikiri ni filamu ya katuni ya Tom na Jerry, maana watani wa jadi Yanga na Simba, jana mchana wamekuwa wakikimbizana kila mmoja akimvizia mwenzake.
Hadi tunakwenda mtamboni jana jioni, Yanga ilikuwa katika hatua za mwisho kutaka kuipiga Simba bao kwa kumsajili mshambuliaji Danny Mrwanda, wakati Simba nayo ilikuwa inataka ‘kuwatoboa’ watani wake kwa kumsajili kiungo wao kinda, Kiggi Makasi.
Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kufanya mazungumzo na Mrwanda aliyekuwa anacheza soka la kulipwa nchini Vietnam, lakini Yanga ikaamua kukatiza na kufanya naye mazungumzo ya kina hadi kufikia makubaliano, kila kitu kilitarajiwa kumalizika jana.
Huku wakiwindana, Simba tayari ilifanya mazungumzo na Kiggi kwa siku mbili mfululizo na jana jioni ilitarajia kumaliza kila kitu ili Kiggi awe mali yao.
“Kweli tumezungumza na Kiggi, kila kitu kitakamilika leo. Amekubali kuichezea Simba, tunamalizia masuala fulani kidogo,” kilieleza chanzo cha uhakika kutoka Simba lakini kikiwa na hofu kama Yanga watajua mchezo huo mapema, wanaweza kuweka kigingi.
“Unajua Simba wana maneno sana, sisi tunamalizana na Mrwanda leo hii (jana), halafu waache waendelee kupiga kelele,” kilieleza chanzo kutoka Yanga.
Viongozi wa kila upande walionekana wakihaha mchana kutwa, huenda wachezaji wote hao wangemwaga wino mapema lakini kifo cha mwanamichezo Ally Suleiman ‘Aurora’ kilikwamisha mambo baada ya kila upande kuungana kwenye makaburi ya Kisutu kwa ajili ya kumsindikiza.
Habari za uhakika, zinaeleza jana saa 9 Alasiri, Kiggi alionekana eneo la Kurasini, Dar es Salaam, katika ofisi za Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye hata hivyo aligoma kulizungumzia suala hilo kwa madai yuko mkutanoni.
Jana saa 10 jioni, kiongozi mwingine wa Simba akaliambia Championi Jumatano: “Dau letu na Yanga limelingana na Mrwanda amekiri kufuatwa na Yanga, lakini amekubali kuchezea kwetu maana ndiyo timu anayoipenda.”
Mrwanda alianza ‘kuosha’ nyota yake baada ya kutua Simba akitokea AFC ya Arusha miaka sita iliyopita, baada ya hapo aliendelea kupasua mawimbi kisoka kwa kucheza soka katika nchi za Rwanda, Kuwait na Vietnam.
Tayari Yanga imemsajili ‘best friend’ wake, Nizar Khalfan na ilionekana Yanga walizoza naye ili asaidie kazi ya kumsogeza winga huyo mwenye kasi ili aongeze nguvu Jangwani.
Simba imekuwa ikifanya hivyo kwa lengo la kulipa kisasi baada ya kipa wake namba mbili, Ally Mustapha ‘Barthez’ kutua Yanga ‘bila taarifa’.
Hali ilivyokuwa inakwenda, huenda mambo yangeweza kubadilika na timu moja ikabeba wachezaji wote na nyingine kubaki tupu au wakagawana mchezaji mmoja mmoja.
Usajili umeonekana kuwa moto baada ya Yanga kumaliza mgogoro na vigogo kuanza kujitokeza tayari kusaidia usajili wa timu hiyo. Ndani ya kamati za usajili za timu hizo hakuna anayelala.
0 Comments