Manuel Preciado |
Kocha mpya aliyeteuliwa juzi Manuel Preciado amefariki saa 24 baada ya kutangazwa kama Kocha wa klabu ya Uhispania, Villarreal.
Kocha huyo ambaye hapo zamani alikuwa kocha wa Sporting Gijon alifariki kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 54.
Kifo chake kimetokea saa 24 baada ya kukubali mkataba wa kuiongoza klabu ya Villareal iliyoshuka daraja, ambapo mkataba wake ulikuwa wa kuanza msimu wa mwaka 2012 hadi 2013.
Preciado alifutwa kazi na Sporting Gijon mnamo mwezi Januari licha ya kuiwezesha klabu hiyo kupanda daraja mara mbili kuingia Ligi kuu ya Uhispania, La Liga.
Mnamo mwezi Aprili mwaka 2011, klabu yake ya Sporting Gijon iliikwamisha klabu maarufu ya Real Madrid kwa kuvunja rekodi yake ya miaka tisa bila kupoteza kwenye uwanja wa nyumbani safari hii ikiwa chini ya Jose Mourinho.
Wakati wake wa uchezaji soka Preciado alicheza kama beki aliyeanzia uchezaji wake katika klabu ya Racing Santander na pia kushiriki mechi za vilabu kama Linares, Mallorca, Alaves, Ourense na Gimnastica.
Baada ya kustaafu kama mchezaji mwaka 1992, akaanza shughuli za ukufunzi akianzia klabu ya Gimnastica na pia kuifunza Racing B, Racing Santander, Levante na Murcia kabla ya kujiunga na Sporting Gijon mwaka 2006.
Baadaye aliiwezesha klabu hio kupanda daraja hadi Ligi kuu ya Uhispania katika msimu wake wa pili na kukaa na klabu hio kwa kipindi cha miaka sita.
0 Comments