Na Khamis Haji, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka Wazanzibari kuendelea kudumisha amani na usalama na kuepuka vitendo vitakavyochangia uchumi wa nchi na hali za kimaisha za wananchi kuporomoka.
Alisema wananchi na wakaazi wote wa Zanzibar lazima wafahamu Utalii ndio shughuli kuu ya kiuchumi inayoongoza katika kulipatia taifa fedha za kigeni, hivyo waendeleze tabia ya ukarimu, upole na waepuke vitendo vinavyoweza kuwakimbiza watalii.
Alisema hayo jana wakati akifungua warsha juu ya utekelezaji wa dhana ya ‘Utalii kwa Wote’ Zanzibar, inayofanyika hoteli ya Manta Resort, Makangale mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Utalii ni shughuli nyeti sana, iwapo kutakuwa na vitendo vya ukabaji, unyang’anyi au usumbufu wa aina yoyote ile, mtalii hatarudi tena. Lakini baya zaidi atatangaza kuwa nchi hii sio salama kwa kutumia vyombo vya habari na mtandao wa intanet”, alionya Maalim Seif.
Alisema kwa zaidi ya miaka 20 sasa tokea serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukaribisha vitega uchumi, lakini bado wananchi wengi hawajanufaika kama ilivyokusudiwa, na ndio maana serikali ikabuni utaratibu mpya wa “Utalii kwa Wote” kuwanufaisha wananchi walio wengi zaidi.
Maalim Seif alizihimiza taasisi zinazohusika na utalii kuwaelimisha na kuwashajiisha wananchi katika shughuli za kuendeleza mbele utalii, kama zinavyofanya baadhi ya nchi zilizopata mafanikio makubwa kwenye sekta hiyo.
“Ukienda Bali, Indonesia utakuta wananchi wote wanafanya shughuli zenye uhusiano na utalii, iwe kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara na hata viwanda”, alisema Maalim Seif.
Akizungumzia utalii katika kisiwa cha Pemba, alihimiza kuepukwa kasoro zilizojitokeza katika kisiwa cha Unguja, wakati wa kuanzishwa sekta hiyo.
Alieleza miongoni vya kasoro hizo ni ujenzi wa hoteli usio zingatia sheria na kanuni za mazingira na kuhimiza taasisi na wadau wa utalii kuweka mkazo mkubwa wa kupata watalii wanaoheshima mila na silka za watu, ili kuepusha kuvurugika kwa maadili.
Maalim Seif alisema visiwa vya Zanzibar vina utajiri mkubwa wa maliasili, yakiwemo matumbawe na vitu vya kale, na kuonya iwapo wananchi na wawekezaji wataendeleza vitendo vya uchafuzi na uharibifu wa mazingira, utajiri huo utapotea.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema mkakati wa ‘Utalii kwa Wote’ unalenga kuwanufaisha wananchi wote na utalii kutokana na shughuli wanazozifanya kujiingizia kipato.
Alisema hatua mbali mbali za kuandaa mazingira bora kwa sekta hiyo zimechukuliwa, ikiwemo kuimarisha miundo mbinu ya barabara, kupeleka umeme wa uhakika katika kisiwa cha Pemba na sasa juhudi kubwa zinaendelea kuchukuliwa kupata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote.
Mtaalamu kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ayoub Khamis Abdalla akiwasilisha mada juu ya ‘Utalii kwa Wote’ alisema hadi sasa utalii katika kisiwa cha Pemba uko nyuma, ikilinganishwa na kisiwa cha Unguja, na kwamba juhudi zinahitajika kuinua sekta hiyo na kuwanufaisha wakaazi wake.
Alieleza kuwa hadi mwaka 1980 Pemba kulikuwa na hoteli tatu tu, lakini baada ya kuundwa Kamisheni ya Utalii mwaka 1992 mambo yamebadilika na sasa hoteli hizo zimefikia 15, nyumba za kulala wageni sita, ambapo hivi sasa kuna jumla ya vyumba 216, vitanda 383 na ajira ya watu wasiopungua 256.
0 Comments