Na Elvan Stambuli
JAMII ya Siri (Secret Society), Freemason, imedaiwa kuwa na siri nzito na viongozi wakuu wa nchi yetu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Madai hayo, yametokana na kile kinachoonekana kwamba Kiongozi Mkuu wa Freemason, Afrika Mashariki, Sir Andy Chande, amekuwa akijiweka karibu na viongozi wakuu wa nchi hii kila awamu, hivyo kuonesha kuwa kuna kitu anakitafuta.
Kikubwa kinachodaiwa ni kuwa Chande anatumiwa na Freemason kuhakikisha kwamba kila kiongozi wa nchi hii anakuwa karibu na jamii hiyo ya siri.
Inazidi kudaiwa kuwa Freemason inafanya njama za hali ya juu kujiweka karibu na Ikulu, ikiwa na mpango wao wa muda mrefu wa kusimika rais ambaye ni memba wa jamii hiyo katika awamu zinazokuja.
Uchunguzi wa Uwazi umeonesha kuwa Chande amekuwa karibu na Ikulu tangu Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na amedumu kujiweka karibu na viongozi wa nchi mpaka awamu hii ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Wakati inabainishwa hivyo nchini, wachambuzi wa mambo ya jamii za siri, ikiwemo Illuminati na Skull & Bones, wamekuwa wakiitaja Freemason kuwa na njama za kuitawala dunia kwa kuhakikisha kwamba kiongozi mkuu wa kila nchi duniani anakuwa memba wa jamii hiyo.

MKAPA
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alipokuwa madarakani aliwahi kualikwa akiwa na mkewe katika shughuli ya Freemasons kutimiza miaka 100 nchini, sherehe iliyojumuisha wageni waalikwa 350 kutoka nchi mbalimbali duniani japokuwa hapa nchini haikutangazwa sana.
Kwa mujibu wa Sir Andy Chande katika mahojiano yake na mwandishi mkongwe nchini, Ernest C. Ambali wa Gazeti la The Guardian, lililokuwa mitaani Oktoba 8, 2004 alitaja waziwazi kuwa mgeni rasmi katika shughuli yao ni Rais Benjamini Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa. Katika shughuli hiyo pia walikuwepo wafanyabiashara wakubwa,wanadiplomasia, mawaziri n.k.
NYERERE
Sir Andy Chande akiwa nchini India katika Mji wa Chennai kuzindua hekalu lao la East Star, alieleza kwamba marais wawili wa kwanza wa Tanzania hawakuwa Freemasons lakini walifahamu taasisi hiyo ni nini na inafanya nini katika nchi hii.

Aidha, aliwahi kuweka wazi kuwa hata Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akiijua taasisi hiyo na aliwahi kuikingia kifua ilipotaka kunyang’anywa jengo lao ambalo lipo Sokoine Drive, katikati ya Jiji la Dar es Salaam linalofahamika kama Freemasons Hall.Uchunguzi umeonesha kuwa viongozi wengi wakuu wa serikali wanafahamu shughuli za taasisi hiyo, hali iliyothibitishwa na kiongozi wa Freemasons, Sir Chande ambaye amekuwa akipiga nao picha mara kwa mara wakati wa hafla.
Viongozi wengine wa nchi waliowahi kualikwa au kumualika kiongozi wa taasisi hiyo ni Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Rais Mstaafu, Sheikh Ally Hassan Mwinyi.

KITABU CHAKE
Rais mstaafu, Mkapa katika kitabu cha Sir Andy Chande kiitwacho ‘Shujaa wa Afrika, Safari kutoka Bukene’ ameandika utangulizi akisema Chande alikuwa akijulikana kama JK na alifahamiana naye baada ya kumuingiza katika bodi ya Shule ya Shaaban Robert.
Mkapa amesema Sir Chande ametambuliwa na kupewa heshima na vyombo vya taifa na vya kimataifa, heshima ambayo anaistahili kabisa. “Mimi nafurahi kuhusishwa na kutambuliwa kwa sifa na heshima anayopewa,” alisema Mkapa katika maandishi yake.
Mnajimu maarufu nchini, Maalim Hassan Yahya Hussein ambaye amekuwa akiandika makala za Freemasons katika gazeti hili, alipohojiwa na mwandishi wetu kama viongozi hao wanafahamu taasisi hiyo inajishughulisha na nini, alisema japokuwa hakuna anayejua wanachokifanya wanachama wa Freemasons huku uraiani lakini anaamini kuwa viongozi wakuu wa nchi wanajua kila kitu.“Kwa kawaida huwezi kualikwa katika chama au taasisi fulani bila kujua shughuli zao hasa kwa viongozi wakuu kama hawa, sasa kama waheshimiwa Mkapa, Mwinyi, Sumaye, Karume na Kikwete waliwahi kualikwa au kumualika Sir Andy Chande ni wazi kuwa wanafahamu shughuli zake na taasisi yake,” alisema Maalim Hassan.
KIMATAIFA
Hivi karibuni, nchini Kenya, aliyekuwa Waziri wa Usalama, Profesa George Saitoti aliyefariki kwa ajali ya helikopta, kifo chake kimehusishwa na Freemasons kwa kudaiwa kuwa alipokuwa Makamu wa Rais wa Kenya wakati wa utawala wa Daniel Arap Moi, aliwahi kupiga marufuku makanisa au dini zinazojihusisha na imani za kishetani.
Imeelezwa kuwa wengi wanadhani kuwa angeweza kuwa Rais wa Kenya iwapo angegombea hivyo kurejesha amri yake ya kupiga marufuku imani ambayo yeye haiamini.
Aidha kuna baadhi ya viongozi duniani wanahusishwa na Freemasons baada ya kuonekana picha zao wakionesha alama za taasisi hiyo, baadhi yao ni Rais Barack Obama, George Bush, Sadam Hussein na Muammar Ghaddafi.