Mchezaji Tyson Lyoka (kushoto) wa timu ya soka ya shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa akichuana vikali na Goodluck Mabiki (kulia) wa shule ya Msongola katika moja ya mechi za ufunguzi wa michuano ya 'Airtel Rising Stars', uliofanyika katika uwanja wa Airwing. Msongola ilishinda 4-0. (Picha na Mpiga Picha wetu)


--
Michuano Airtel Rising Stars yaanza Dar, Mbeya na Arusha
Michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars 2012 imeanza rasmi jana ngazi ya mkoa kwa shule ya Sekondari ya Msogola kuisambaratisha bila huruma shule ya Benjamin Mkapa 4-0 kwenye mchezo uliocheza kwenye uwanja wa shule ya Airwing, jijini Dar es Salaam.
Kwenye mchezo huo ambao ulikuwa ni ufunguzi kwa mkoa wa kisoka wa Ilala, magoli ya Msogola yalifungwa na Dickson Alphonce dakika 62, Abdul Saidi 67, Hanica Seleman 86 na Goodluck Mabiki akapigia msumari wa mwisho dakika ya 87.
Kwa Mkoa wa kisoka wa Temeke, shule ya sekondari ya Tirav ilitoka sare ya 2-2 na shule ya Kurasini, mchezo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Twalipo na kufurika mamia ya mashabiki huku wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kurasini. Mchezo huo ulianza taratibu huku kila timu ikitaka kusoma mbinu za mwenzake na kuongeza kasi ya mchezo kadri muda ulivyokuwa unasonga.
Shule ya Tirav ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao, ambalo lilipatikana kwa mkwaju wa penati kwenye dakika ya sita ya mchezo baada ya kipa wa Kurasini kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Tirav, Paul Balama kwenye eneo la hatari. Paul Balama ndio alifunga penati hiyo huku akimwacha golikipa wa Kurasini akiwa hana la kufanya.
Baada ya goli hilo, Kurasini ilifanya mashambulizi mfululizo na kwenye dakika la nane, Justin Macha aliisawazishia timu yake baada ya kazi nzuri kati yake na Awadh Mtawamba na Muhalami Ally. Goli hilo liliamsha shangwe na vishindo kwa mashabiki wa shule ya Kurasini huku wengi wakiwemo wanafunzi wenzao.
Shule ya Tirav ilipata goli ya pili kupitia kwa Paul Balama ambaye alikuwa ni mwiba mkali kwa ngome ya Kurasini kwenye dakika ya 19 huku Kurasini wakisawazisha kwenye dakika ya 85 na kufanya uwanja wote kulipuka kwa shangwe na nderemo.
Kwenye mechi nyingine ya ufunguzi kwenye mkoa wa Kinondoni, Shule ye sekondari ya Twiga iliifunga shule ya Mpiji Magohe 1-0 huku goli la kipekee likiwekwa kimiani na Louis Andrew kwenye dakika la 35 ya mchezo.
Mkoani Mbeya, Shule ya sekondari ya Mbeya Day ilikuwa na kila sababu ya kufurahi baada ya kuichapa Wenda sekondari 2-0 kwenye mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine, huku katika mkoa wa Arusha, shule ya Kaloleni ikiisambaratisha bila huruma Sinoni Sekondari kwa 5-0.