Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam,Mh. Said Meck Sadik akikabidhi Bendera kwa Nahodha wa timu ya taifa (Taifa Stars),Juma Kaseja kwa ajili ya safari yao ya kwenda kuiwakilisha nchi katika mchezo wao dhidi ya Msumbiji (The Mambas) utakaochezwa Jumapili (Juni 17 mwaka huu) ikiwa ni kuwania tiketi ya kucheza kombe la Dunia mwaka 2014.katikati ni Kocha wa Taifa Stars,Kim Paulsen na Mkuu wa msafara ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF,Shaibu Nampunde.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam,Mh. Said Meck Sadik akipeana mkono na Nahodha wa timu ya taifa (Taifa Stars),Juma Kaseja mara baada ya kukabidhi bendera kwa timu hiyo ambayo inaondoka kesho kwenda Msumbiji .
Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa wakifuatilia hotuba fupi ya Mkuu wa Mkoa wa wakati wa Hafla fupi ya kuwakabidhi bendera ya taifa,jijini Dar es Salaam leo.



Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki ameitaka timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kuiwakilisha vyema nchi katika mchezo wake dhidi ya Msumbiji (The Mambas) utakaochezwa Jumapili (Juni 17 mwaka huu).

Ametoa mwito huo leo (Juni 14 mwaka huu) wakati akimkabidhi nahodha wa timu hiyo Juma Kaseja, Bendera ya Taifa tayari kwa safari ya kwenda Msumbiji itakayofanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) asubuhi. Stars itaondoka kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.

RC amesema kiwango ambacho kilioneshwa na Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwenye mechi dhidi ya Ivory Coast na Gambia kimerudisha imani ya Watanzania kwa timu hiyo, hivyo kuwataka wachezaji kuendeleza moto huo.

Aliwataka wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi kupigana kiume kuhakikisha wanashinda mechi hiyo, kwani ushindi mbali ya kuwaingiza katika raundi inayofuata pia utaifanya Tanzania ipande kwenye orodha ya viwango vya ubora duniani inayotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa ulioko Zampeto nje kidogo ya Jiji la Maputo kuanzia saa 9 kamili mchana kwa saa za huko.

Waamuzi hao ni Hamada Nampiandraza atakayepuliza filimbi, Alberto Razafitsatamy, Paulo Andriovoavonjy na Bruno Andriamiharisoa. Kamishna wa mechi hiyo kutoka Botswana ni David Fani.

Taifa Stars inaondoka na msafara wa watu 32 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Msafara huo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Shaibu Nampunde.