Rais wa Ujerumani Angela Merkel akizungumza na waandishi wa habari
Viongozi wa Ulaya wamekubaliana kimsingi kutumia dola bilioni 150 katika hatua za dharura za kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Lakini Uhispania na Italia zinasema haziwezi kutia saini mpango huo, hadi hapo nchi zingine za Muungano wa Ulaya zitakapoahidi kuzisaidia nchi hizo kukabiliana na madeni yake zikiwemo gharama za ukopaji.

Akizungumza mwishoni mwa siku ya kwanza ya kikao cha viongozi wa Muungano wa Ulaya mjini Brussels, rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema anataka suluhisho la haraka kwa nchi za Euro zinazokabiliwa na madeni makubwa.

Ujerumani yatofautiana


Hata hivyo Ujerumani inasisitiza kuharakishwa kwa umoja wa kisiasa na kifedha kabla haijakubali kugawana deni linalozikabili nchi wanachama.

Mpango huo umependekeza mambo mengi kama vichocheo vya uwekezaji katika mataifa hayo. Kama vile, kutumia pesa ambazo zimehifadhiwa katika bajeti za nchi za bara Ulaya, kuzisaidia benki za Ulaya za uwekezaji, na kutoa mikopo kusaidia nchi zenye matatizo ya kiuchumi.

Mipango hiyo haihusishi kuondoa mipango iliyowekwa ya kupunguza matumizi ya serikali kwa mataifa yanayopata misaada ya kifedha.

Wakosoaji wamesema mipango ya sasa haitakuwa na mchango mkubwa katika kutatua matatizo yanayokumba mataifa yanayotumia sarafu ya Euro.

Mzozo wa kifedha wa mataifa hayo ni mada itakayoendelea kujadiliwa katika mkutano huo wa viongozi kutoka Ulaya.

Italia na Uhispania


Bado, hakuna dalili yoyote ya kutatua kutoelewana kuhusu iwapo kunahitajika kuchukua hatua za haraka kupunguza gharama ya mikopo ya nchi za Italia na Uhispania.

Kiongozi wa Ujerumani Angela Merkel anapinga mipango hiyo ya kuzipunguzia nchi hizo gharama ya mikopo akidai itakuwa ni kitisho kwa raia wa nchi yake wanaolipa kodi.