Na Makongoro Oging'
HATIMAYE Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Kikosi cha Kupambana na Madawa ya Kulevya limemnasa mume wa ndoa wa Miss Mzizima na Mshiriki wa Miss Tanzania 2005 ambaye sasa ni modo, Jacqueline Patrick ‘Jack’, Abdullalatif Fundikira, UWAZI linaanika sinema nzima.
Kutiwa mbaroni kwa Fundikira kumethibitishwa na kamanda wa kikosi hicho, Godfrey Nzowa alipozungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita ofisini kwake, Kilwa Road Jijini Dar es Salaam.
KWA NINI ALINASWA?
Kamanda Nzowa alisema kuwa jeshi lake limelazimika kumkamata Fundikira baada ya kuwa katika orodha ya watu waliotajwa kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya.
SINEMA YA KUNASWA KWAKE
Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo alidakwa nyumbani kwake, Mbezi Beach, Kinondoni Jijini Dar es Salaam saa 12.00 asubuhi.
“Fundikira tulimkamata nyumbani kwake, ilikuwa saa kumi na mbili asubuhi. Kwa sasa tunamshikilia na upelelezi unaendelea, utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema Kamanda Nzowa.
Akaongeza: “Fundikira alikuwa akitafutwa na jeshi tangu Mei 16 mwaka huu baada ya kutajwa na mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la Mariam Mohamed Said, 29, kuwa ni miongoni mwa wauza madawa ya kulevya.
“Huyu mwanamke alinaswa katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere katika operesheni ya polisi ya ‘kufagia’ mtandao wa madawa ya kulevya.”
Kamanda Nzowa alisema Mariam alikamatwa akiwa na begi lenye uzito wa kilo 10 likiwa na mabunda 23 ya bangi yenye thamani ya shilingi milioni 12. Alikuwa akienda nchini Uturuki.
Alisema mara baada ya mwanamke huyo kunaswa, alimtaja Fundikira kuwa ‘memba’ wa mzigo huo. Ndipo jeshi la polisi lilianza kumtafuta mtuhumiwa hadi nyumbani kwake lakini akawa anajificha.
Akasema: “Hatimaye Jumamosi (Juni 9, 2012) alikamatwa kwa ushirikiano wa askari wangu na raia wema.”
AKUTWA JUU YA DARI
Habari zaidi za kipolisi mbali ya Kamanda Nzowa zilisema kuwa saa 11:00 alifajiri ya siku ya tukio, kikosi kazi kinachoongozwa na kamanda mwenyewe kiliizingira nyumba ya Fundikira na baada ya dakika kadhaa polisi waligonga geti.
Ikadaiwa kuwa mlinzi wa mtuhumiwa huyo alileta mvutano kati yake na polisi lakini hata hivyo, hakufua dafu kwani maafande hao waliingia ndani na kumsaka mtuhumiwa ingawa bila mafanikio.
Habari zikazidi kudai kuwa polisi walimkuta mke wa mtuhumiwa, Jack Patrick (pichani) ambaye naye alipobanwa aseme alipo mumewe huyo, hakutaka kutoa ushirikiano badala yake akawa anatetemeka.
Baadaye walisikia kitu kikitambaa kama nyoka juu ya dari, wakawa na shaka nako, walipozamia walimkuta mshukiwa huyo amejificha hivyo kumchomoa na kumpiga pingu hadi kwa mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo.
Baada ya kukamilisha taratibu za kiserikali kwa mjumbe huyo, Nzowa na maafande wake walimfikisha mtuhumiwa Makao Makuu ya Kitengo cha Madawa ya Kulevya kilichopo Kilwa Road Jijini Dar es Salaam.
WASIWASI WA UTAJIRI WAIBUKA
Habari zaidi zilieleza kwamba, mtuhumiwa alihojiwa kuhusu nyumba ya ghorofa moja anayoishi kama ni yake ambapo alijibu amepanga na amekuwa akiilipia shilingi laki saba kwa mwezi (shilingi 8,400.000 kwa mwaka).
SHUKURANI KWA WANANCHI
Aidha, kwa upande wake, Kamanda Nzowa aliwashukuru raia wema kwa ushirikiano walioutoa katika kufanikisha kunaswa kwa mtuhumiwa huyo, akawaomba waendelee na moyo huo ili jeshi lake liweze kupambana na waovu wote.
TAHADHARI
Kwa upande mwingine, Nzowa aliwatahadharisha wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya kuacha mara moja kwani jeshi lake limejipanga vizuri kukabiliana na wahusika.
MAWAKILI MIDOMO WAZI
Katika Gazeti la Ukweli na Uwazi No. 739 la Mei22-28, 2012 ukurasa wa mbele kulikuwa na habari ya pili yenye kichwa; MADAI YA POLISI; MUME WA JACK PATRICK MUUZA UNGA.
Ndani ya habari hiyo, Kamanda Nzowa alithibitisha kuwa, jeshi lake linamsaka Fundikira kwa madai (kama kichwa cha habari kilivyosema, madai) kujihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya.
Baada ya habari hiyo kutoka hewani, Fundikira kupitia mawakili wake waliliandikia Uwazi barua ya kisheria wakidai kuwa habari hiyo haikuwa ya kweli na ilikuwa na lengo la kumchafulia jina mteja wao kwa kuwa hatafutwi na jeshi la polisi.
Aidha, katika barua hiyo, wanasheria hao walilitaka gazeti hili (LA KUFICHUA MAOVU) kumwomba radhi mteja wao sanjari na kulipa fedha kiasi cha shilingi milioni mia sita (600,000,000) kama fidia.
SHERIA IKO WAZI
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jeshi la polisi linaweza kumkamata mtu kwa tuhuma yoyote ile ambapo baada ya upelelezi kukamilika, humfikisha mahakamani au kumuachia huru wakiona hana kosa.
Endapo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani na ikamuona hana hatia, ina uwezo wa kumwachia lakini bila kulaumu jeshi la polisi.
WANA HABARI NA KAZI YAO
Kwa kawaida vyombo vya habari vina uhuru wa kuandika habari zinazotolewa na jeshi la polisi katika ngazi husika, kama lilivyofanya Gazeti la Uwazi, bila kubughudhiwa na mtuhumiwa au mwanasheria wake.
Chanzo changu toka hapa.
0 Comments