Mkuu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko Olivary Kamili akiangalia wanafunzi wakijipanga tayari kuingia madarasani kuanza masomo. (Picha na Nathaniel Limu).

Na Nathaniel Limu.
Serikali ya Tanzania imeombwa kuangalia uwezekano wa kubadili mfumo wa utoaji wa elimu katika vyuo vya ualimu kwa kuongeza elimu maalum, ili kila mwalimu anayehitimu awe na elimu inayojumuisha pia elimu maalum.
Elimu maalum ni ambayo itamsaidia kila mwalimu atakapoingia katika kazi ya ufundishaji, aweze kufundisha kwa ufasaha watoto wote wenye ulemavu na wasio na ulemavu.
Wito huo umetolewa na mwalimu mtaalam wa wanafunzi wasioona wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko iliyopo jimbo la Singida Mashariki Olvary Kamili wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema hatua hiyo pamoja na mambo mengine, itasaidia kuondoa upungufu mkubwa wa walimu wenye sifa na uwezo wa utoaji wa elimu jumuishi (kwa watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu).
“Sambamba na kubadili mfumo, pia elimu itolewe kwa wazazi/walezi juu ya umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shuleni na wazazi/walezi hao waelimishwe kuwa watoto wenye ulemavu, wana haki yakupata elimu sawa na wale wasiokuwa na ulemavu” amesema na kuongeza;
“Elimu jumuishi pia haina budi kutolewa kwa watu wenye ulemavu, ili wawe na utayari wa kushiriki katika mfumo huo wa elimu”.
Shule ya msingi mchanganyiko ya Ikungi ina wanafunzi walio na mahitaji muhimu (walemavu wenye uoni hafifu, ulemavu wa ngozi, albinoi) jumla yao ni 81.