Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, Linus Vicent Sinzuma akitoa taarifa ya kifo cha mwanamke mmoja kufia kwenye nyumba ya kulala wageni ya Pesaba ya mjini Singida kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha).(Picha na Nathaniel Limu).

Mwanamke mkazi wa mtaa wa Ukombozi kata ya Majengo mjini hapa mwenye umri wa miaka 35, amefariki dunia kwenye nyumba ya kulala wageni ya Pesaba.
Mwanamke huyo ambaye inadaiwa alikuwa akifanya biashara ya kuuza mwili, ni Jamila Haji.
Akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Linus Vicent Sinzumwa, alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia juzi juni 12 mwaka huu, nyakati za usiku.
Alisema siku ya tukio, Rashidi Hassan aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa mkoa wa Mara, alipanga kwenye nyumba hiyo ya Pesaba chumba No. 3 B, ghorofa ya kwanza.
Alisema mpangaji huyo baada ya kutoka kwenda matembezini, usiku saa nne, alirejea akiwa na Jamila.
“Mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni, Mwanahamisi Abdala, wakati akifanya usafi saa sita mchana, aligundua kufariki dunia kwa Jamila na kutoa taarifa kituo cha polisi, Singida mjini”,alisema Sinzumwa.
Alisema askari polisi baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa Jamila, hawakuona jeraha lo lote, zaidi ya povu jeupe mdomoni. Pia zilikutwa chupa tatu tupu za bia na chupa moja kubwa ya maji.
Kuhusu mpangaji Rashidi, kamanda huyo alisema mhudumu huyo amedai kuwa mpangaji huyo alitoka saa 12:00 asubuhi na haijulikani alikoelekea. Alimwacha Jamila akiwa amelala kitandani.
“Kwa sasa tumeanzisha msako mkali wa kumsaka mwanaume huyo aliyelala na Jamila, ili tuweze kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria. Vile vile tunasubiri uchunguzi wa daktari ili tuweze kujua ni kitu gani hasa kilichosababisha kifo cha msichana huyo”,alisema.
Mmoja wa wahuduma wa nyumba hiyo ya kulala wageni ya Pesaba, ambaye amekataa jina lake kutajwa humu gazetini, alisema wakati wanatoa mwili wa Jamila chumbani, walikuta kondomu saba zilizotumika zikiwa zimezagaa sakafuni. Pia chini ya mto wa kulalia, kulikuwa na kondomu nne ambazo hazijatumika.