Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,Linus Vicent Sinzuma akitoa taarifa ya kifo cha kilichohusishwa na ugomvi wa shamba kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha).Picha na Nathaniel Limu.
Mkulima mkazi wa kitongoji cha Mkunguu kijiji cha Kinyeto tarafa ya Ilongero wilayani Singida, mzee Rajabu Hongoa (62), amefariki dunia baada ya kukatwa katwa kwa panga.
Mauaji hayo ya kusikitisha na ya kinyama, inadaiwa yametokana na ugomvi wa muda mrefu wa kugombea shamba.
Akizungumza ofisini kwake , Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Linus Vicent Sinzumwa, alisema tukio hilo limetokea juzi saa tisa alasiri katika kijiji cha Kinyeto.
Alisema mzee huyo siku ya tukio wakati akirudi nyumbani kwake baaada ya kumsindikiza mgeni wake, alikutana njiani na kijana Ramadhani Juma (22).
“Walipokaribiana,ghafla Kijana Ramadhani alianza kumkata kata kwa panga mzee Hongoa sehemu mbali mbali za mwili, na kumsababishia majeraha ambayo yalipelekea kuvuja damu nyingi. Mzee huyo baada ya kuvuja damu, alianguka chini na kisha kufariki dunia papo hapo”,alisema.
Akifafanua, Sinzumwa alisema Juma Swalehe ambaye ni baba yake na kijana Ramadhani Juma, waliwahi kushitakiana mahakamani kutokana na kugombea shamba hilo.
“Lakini hata hivyo,marehemu Hongoa, alimshinda Juma Swalehe, na hivyo mahakama ilihalalisha kuwa shamba lililokuwa likigombewa, ni mali halali ya Hongoa”,alifafanua.
Kamanda huyo, alisema baada ya maamuzi hayo ya mahakama, familia ya Juma Hongoa ilimchukia mzee Rajabu Hongoa na kuanza kumfanyia visa vya kumuuwa.
“Kwanza alianza kaka yake na Ramadhani Juma, Adamu katika siku za nyuma. Adamu aliwahi kumshambulia mzee Hongoa kwa panga, lakini lengo lake la kumuuwa mzee huyo halifanikiwa. Baada ya kushindwa kutimiza azma yake hiyo, alitoroka na hadi sasa haijulikani amekimbilia wapi”,alisema kamanda Sinzumwa.
Alisema hivi sasa wameanzisha msako mkali wa kuwasaka Adamu na mdogo wake Ramadhani Juma, ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Wakati huo huo,Kamanda Sinzumwa ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wachukue taratibu za kisheria katika kutatua kero zao mbalimbali.
0 Comments