Na.Mohammed Mhina na Pardon Mbwate, wa Jeshi la Polisi
Makachero wa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma jana walilazimika kutumia risasi kupambana na kundi la majambazi wenye silaha waliokuwa wamepanga kumvamia mmoja wa wafanya biashara mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma ACP. Frasser Kashai (Pichani), amesema kuwa katika tukio hilo Polisi walimpiga risasi mmoja wa majambazi hayo aliejulikana kwa jina la Lowasi Moria(22) mkazi wa Kijiji cha Kabale mkoani humo.
Kamanda Kashai amesema wakati wa mapambano hayo, majambazi wengine watatu walifanikiwa kutoroka huku wakimuacha mwenzao aliyekuwa na silaha hiyo aina ya SMG akiwa anagaragara chini kutokana na majeraha ya risasi.
Hata hivyo Kamanda Kashai amesema jambazi huyo aliyekuwa na SMG yenye namba TU 8453 ikiwa na risasi nne zilizobaki kwenye magazine yake alifariki dunia wakati Polisi walipokuwa wakimpeleka Hospitali kwa matibabu.
Kamanda kashai amesema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 06.00 mchana huko kwenye pori la Ruhuru lililopo karibu ya kijiji cha Gwarama wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.
Amesema Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna majambazi yenye silaha na wamepanga kuwavamia wafanyabiashara wanaopita katika eneo hilo na ndipo askari waliokuwa wakifanya doria katika barabara hiyo walipoamua kuweka mtego katika eneo hilo.
Kamanda huyo amesema kuwa, wakati wakiwa katika eneo hilo, Polisi walimuona mtu mmoja akiwa na pikipiki akitokea Kakonko kwenda Muhange Kabale na baada ya muda si mrefu majambazi hayo walijitokeza na kumvamia na ndipo walipoanza kurushiana risasi na kufanikiwa kumjeruhi mmoja wao.
Katika tukio lingine Kamanda Kashai amesema juzi majira ya saa nne usiku huko kwenye eneo la Mwanga mjini Kigoma, dereva mmoja wa bodaboda aitwaye Puldence Gasto(28), mkazi wa Majengo alimwagiwa tindikali usoni na abiria aliyembeba kisha kumpora pikipiki yake.
Kamanda huyo ameitaja pikipiki iliyoporwa kuwa ni yenye namba T 692 BLZ aina ya SUNLG, rangi nyekundu ambayo hadi sasa haijajulikana mahali ilipo.
Amesema dereva huyo wa bodaboda amelazwa kwenye hospitali ya mkoa ya Maweni kwa matibabu zaidi wakati Polisi wakiendelea na msako dhidi mtuhumiwa pamoja na pikipiki hiyo.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Kashai, ametoa wito kwa vijana waendesha boda boda mkoani humo, kuwa na ushirikiano na kwamba kila mmoja wao amzingatie abiria aliyechukuliwa na mmoja wao ili iwe rahisi kumkamata linapotokea tatizo kama hilo.
0 Comments