Rais Vladmir Putin wa Urussi amekataa kukubali shinikizo za kibalozi kutoka Mataifa ya magharibi yakiitaka nchi yake kuichukulia hatua kali serikali ya Syria.
Bw.Putin, mshirika mkubwa wa Syria ametaka Syria ipewe mda zaidi kutekeleza mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan.
Marekani na Uingereza zimeitaka Urussi iongeze makali katika kuishutumu Serikali ya Syria kufuatia mauwaji ya wiki iliyopita huko Houla ambako watu 108 waliuawa.
Kabla ya hapo, Urussi ilikua imepinga azimio lililopitishwa na Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.
Kikao cha dharura kilichofanyika siku ya Ijumaa, Baraza hilo liliishutumu Syria juu ya mauwaji ya Houla na kutaka uchunguzi wa kina ufanywe. Lakini Urussi ilipinga azimio lililopendekezwa na Marekani kwa hoja kua lilikua na upendeleo.
Wakati huo huo, wavuti moja ya Marekani imechapisha picha zilizopigwa kupitia satelaiti zikionyesha makaburi makubwa katika eneo la Houla.
Akizungumza mbele ya wandishi wa habari, Bw.Hollande alitaka shinikizo zaidi na vikwazo, na kusema kua suluhisho lililobaki ni kwa Rais Bashar al Assad kujiuzulu.
Bw.Hollande aliongezea kusema kua utawala wa Bw.Assad unaendesha masuala kwa njia isiyokubalika na vitendo vyake vimeifanya isiyofaa kuongoza.
Rais wa Ufaransa alisema kua hakuna njia ya kuepuka balaa hili ila akiondoka madarakani Bashar Assad.
Bw.Putin, hata hivyo, alihoji miito inayomtaka Rais wa Syria ajiuzulu.
"kwanini tuwe na dhana ya kua tukimuondoa madarakani kiongozi aliyepo hivi sasa ndipo atapatikana kiongozi ambaye moja kwa moja atabadili hali ya mambo na kuleta salama" Alisema Bw.Putin.
Alitoa mifano ya yanayoendelea nchini Libya na Iraq na kuuliza Je kuna salama huko? Aliuliza. Putin aliendelea kusema kua Urussi inapendekeza hatua kwa njia ya uhakika na kwa njia iliyo sawa angalau kwa Syria.
Bw.Putin alisema kua jambo la muhimu ni kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Akizungumza mjini Oslo siku ya Ijumaa, Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Bi Hilary Clinton alikaripia Urussi na kusema kua haamini kama msimamo wa nchi hio unafanywa bila upendeleo.
Bi Clinton aliongezea kusema, "tunafahamu biashara ya silaha imekua ikiendelea katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kutoka Urussi kwenda Syria. Tunaamini kua silaha zinazoendelea kutumwa kutoka Urussi ndizo zilizoifanya serikali ya Assad kuzidi kuimarika.
Mnamo siku ya Alhamisi, Maofisa wa nchi za magharibi walithibitisha taarifa kua Meli ya mizigo ya Urussi iliwasilisha silaha nzito kwenyebandari ya Tartus juma lililopita.
Bw.Putin amesisitiza kua Urussi haijaiuzia Syria silaha zinazoweza kutumiwa katika mapigano na raia.
0 Comments