Mbwana Samatta (kushoto) akimtoka beki wa Ivory Coast Alexandre Lolo wakati wa mechi ya kusaka kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika kwenye uwanja wa Felix Houphouet-Boigny, mjini Abidjan.
Na Khadija Mngwai
MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, amesema moja ya zawadi kubwa aliyoipata kutoka kwa straika wa Ivory Coast, Didier Drogba ambaye pia anakipiga kwenye kikosi cha Chelsea, ni mbinu kali za kuwatoka mabeki na kufunga.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Samatta alisema wakati alipocheza na mshambuliaji huyo wiki iliyopita jijini Abdijan katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, aligundua mbinu nyingi alizokuwa akitumia staa huyo na kudai kuwa imekuwa zawadi nzuri kwake kwa kuwa ataifanyia kazi ili awe bora.
“Nimejifunza vitu vingi kutoka kwa Drogba, ni mchezaji mzuri ambaye anajua kucheza na nafasi, wakati mchezo ukiendelea nilikuwa namsoma kwa kumuangalia jinsi anavyocheza.
“Alikuwa makini sana na mjanja katika kuwahi mpira hata kama ukiwa ukiwa juu, anajua utadondokea wapi, hali hiyo ilikuwa ikimpa nafasi kufanya vizuri zaidi, nimejifunza na kuchukua ujuzi kadhaa kutoka kwake,” alisema Samatta.
Aidha, Samatta alisema licha ya kufungwa mabao 2-0 katika mchezo huo, kikosi chao kilicheza kwenye kiwango kizuri kutokana na ushirikiano uliokuwa ukionyeshwa na wachezaji na kudai kuwa wakikaa kwa muda kikosi kitakuwa kizuri zaidi.