Ibrahim Yamola
SIKU moja baada ya Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) kutangaza kufanya mgomo wiki mbili zijazo ikiwa matatizo yao hayatapatiwa ufumbuzi, Serikali imekubali kurudi katika meza ya mazungumzo.

Akizungumza na Mwananchi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hussein Mwinyi alisema baada ya MAT kufikisha taarifa ya kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa wanachama wake na kuikataa kitakachofuta ni kurudi tena mezani na kujadiliana.
Waziri wa Afya Dr.Hussein Mwinyi.
"Tutakutana na viongozi wao na kujadiliana nao, baada ya wanachama wao kuikataa taarifa hiyo kwani watarejesha wanachokitaka wizarani na sisi tutakutana nao na kujadiliana nao," alisema Dk Mwinyi na kuongeza:
“Tutarudi katika meza ya mazungumzo tukae na kuzungumze kwani hakuna linaloshindikana.”
Juzi, wanachama wa MAT walifanya kikao cha ndani na kutoa taarifa kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza madai yao ya nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi, marupurupu, nyongeza ya posho ya wito wa dharura, posho za nyumba na chanjo.

Katika mkutano huo uliowashirikisha madaktari na viongozi wa chama hicho walikubaliana kutangaza mgogoro wa wiki mbili na baada ya hapo kuingia katika mgomo ili kuishinikiza Serikali kuyapatia ufumbuzi madai yao.

Walidai kuwa kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Pinda ilishindwa kuyatatua matatizo yao kwa kigezo kwamba Serikali haina uwezo wa kifedha.

Madaktari hao walilalamika kwamba ahadi iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwenye mkutano wao ya kuhakikisha madai yao yanashughulikiwa kikamilifu wakati alipowataka warejee kazini baada ya mgomo wao Januari mwaka huu, haikutekelezwa.

Katika Mgomo huo uliosababisha wananchi kwa kukosa huduma, Waziri Mkuu Pinda aliwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu Dk Deo Mtasiwa, ambao wanachunguzwa.

Madai mengine ya madaktari hao ilikuwa ni kuwang’oa mawaziri jambo ambalo Rais Kikwete alilitekeleza kwa kutowarejesha kwenye Baraza alilolisuka upya kwa kuteua wengine.