|
Maandamano Misri |
Mahakama kuu ya katiba nchini Misri imesababisha hali ya wasiwasi nchini humo baada ya kutangaza kuwa uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwaka jana ulikuwa kinyume cha katiba na kutaka ufanyike upya.
Uamuzi huo wa mahakama uliotolewa siku mbili kabla ya kufanyika duru ya pili ya kinyang'anyiro cha urais, unalipa baraza la utawala wa kijeshi nguvu za bunge.
Wanaharakati na wanasiasa wamelishutumu jeshi kwa kufanya mapinduzi.
Kulingana na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, uamuzi huo una athari kubwa hasa kwa kuwa umetolewa kabla ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi mwishoni mwa juma, na inamaanisha sasa kwamba mamlaka ya bunge nchini humo yamo chini ya baraza kuu la Kijeshi ambalo lilipewa jukumu la kuongoza Misri katika kipindi cha mpito baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak kung'olewa madarakani.
Pia kwa msingi wa uamuzi huo, Misri haina katiba kwa sasa na haina bunge.
Chama cha Muslim Brotherhood tayari kimeelezea hofu yake kuwa hatua chache ambazo nchi hiyo ilikuwa imepiga kidemokrasia zinazidi kutoweka.
Chama hicho kimeonya kuwa huenda kukazuka vurumai nchini humo hasa iwapo madaraka ya nchi hiyo yatakabidhiwa kwa watu walio na uhusiano na serikali iliopita ya Hosni Mubarak.
Mgombea wa rais kwa tiketi ya chama cha Muslim Brotherhood, Mohammed Mursi, anakabiliana na aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwenye duru ya pili ya uchaguzi inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma na ameelezea kwamba hajaridhishwa na uamuzi huo, akisema,"tutaendelea na safari yetu na tutakuwa waangalifu sana kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu wakati wa shughuli ya upigaji kura. Na iwapo kutakuwepo na udanganyifu, kutakuwa na mapinduzi makubwa dhidi ya wahuni....mapinduzi makubwa dhidi ya wale wanaotetea wahuni...mapinduzi makubwa hadi tutakapopata malengo yetu.''
Hofu kubwa kisiasa kuhusiana na uchaguzi wa mwishoni mwa wiki ni kwamba uamuzi huo wa mahakama utamwacha rais atakayechukua madaraka bila bunge na bila katiba.
0 Comments