Na Khatimu Naheka
UNAWEZA kusema Simba wamepigwa bao katika dakika za mwisho baada ya kiungo Nizar Khalfan kuwageuka na kusaini kwa watani wao, Yanga.
Awali, kiungo huyo alifanya mazungumzo na viongozi wa Simba chini ya mdhamini wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji lakini wakashindwa kukubaliana masuala ya maslahi ili kiungo huyo aliyekuwa akiichezea Klabu ya Philadelphia Union ya Marekani amwage wino Msimbazi.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nizar alisema ameamua kuondoa sintofahamu hiyo ambapo sasa ataonekana rasmi katika michuano ya Kagame mara atakapovaa uzi wa kijani na njano unaotumiwa na Yanga.
Nizar alisema ameshamalizana na Yanga ambapo amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia klabu hiyo huku akisema kikubwa kilichomvutia ni nyota wa timu hiyo, Haruna Niyonzima ambaye amekuwa akimvutia kwa muda mrefu na kutamani kucheza naye katika kikosi kimoja.
“Ni kweli ndugu yangu nimeshasaini Yanga leo (juzi), hivi tunavyoongea natokea Ilala katika ofisi za mmoja wa viongozi wa Yanga kumaliza suala la kusaini kuitumikia timu hiyo, nadhani Mungu akipenda nitaanza kibarua hicho rasmi katika michuano ya Kagame,” alisema Nizar.
“Nimesaini Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja na baada ya kumalizika mwaka huo, tutakaa tena chini na kuangalia nini tunaweza kufanya lakini kikubwa kilichonivutia Yanga ni kuwa na nyota wengi wenye vipaji hasa Niyonzima (Haruna) ambaye kwangu mimi ni mtu ambaye amekuwa akinivutia sana kwa jinsi anavyocheza.”
Kabla ya kujiunga na Yanga kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24, alikuwa akikichezea kikosi cha Philadelphia Union ya Marekani ambapo alijiunga nacho mwaka jana akitokea Vancouver Whitecaps ya Canada ambayo aliichezea michezo 22.