Watu wa Misri wanapiga kura kwa siku mbili, katika duru ya pili ya kumchagua rais mpya atayerithi nafasi ya Hosni Mubarak aliyetolewa madarakani mwaka jana.
Mashindano yanatarajiwa kuwa makali baina ya waziri mkuu wa zamani, Ahmed Shafiq, na Mohamed Morsi wa Muslim Brotherhood.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo anasema hakuna shauku wala foleni ndefu kama zilizoonekana katika duru za awali za upigaji kura.
Anasema Wamisri hawana hamu na wagombea hao wawili wa urais, na baadhi yao wametaka watu wasusie upigaji kura au wazichafue kura zao.
Uchaguzi wa sasa unafuatia hukumu ya mahakama kuwa uchaguzi wa bunge ulikuwa kinyume na katiba, na lazima ufanywe tena.