Calitz na mumewe Bwana Pelizzari baada ya kuachiliwa huru na maharamia
Raia wawili wa Afrika Kusini ambao wamekuwa wakishikiliwa mateka na Maharamia wa Kisomali wameachiliwa huru.

Wawili hao, Bi Calitz na Bwana Pelizzari, ambao ni mtu na mkewe wamekuwa wakizuiliwa nchini Somalia kwa miezi 20.
Waziri wa ulinzi wa Somalia amesema jeshi na walinda usalama walikuwa wameanza harakati za kuwaokoa watu hao siku ya Jumatano usiku.

Bi Calitz na Bwana Pelizzari walitekwa nyara mwezi Oktoba mwaka 2010 walipokuwa ndani ya chombo chao katika bahari hindi.

Hata hivyo Waziri wa ulinzi wa Somalia Hussein Arab Isse hakufichua kama kikombozi chochote kililipwa kabla ya wawili hao kuachiliwa.


Awali maharamia hao walikuwa wametaka kulipwa dola milioni 10 kabla ya kuwaachilia raia hao wawili wa Afrika Kusini.

Mtu huyo na mkewe walijitokeza wakiwa na waziri huyo katika mkutano wa waandishi habari.

Walisema walikuwa na furaha na walikuwa wanatarajia kujiunga na familia yao.

Umoja wa ulaya unasema kwa wakati huu kuna jumpla ya mateka 213 ambao bado wanazuiliwa na maharamia.