Askari wa Kongo wamekimbilia na kuingia nchini Uganda kufuatia
mapigano na waasi, wakazi wa mji wa mpaka wa Bunagana wameiambia BBC.
Wenyeji Bunagana wamesema kuwa askari wengi walikuwa wamevuka mpaka, ambapo
walipokonywa silaha na jeshi la Uganda .
Inaamikia kuwa waasi wemeudhibiti mji huo kwa upande wa Kongo ambao pia upo
upande wa Uganda.
Waasi wa Bosco Ntaganda walibeba silaha na kuanza mapambano katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo mwezi Aprili.
Waasi hao ni wale waliojiondoa katika jeshi baada ya shinikizo kuongezeka kwa
serikali kumkamata Jenerali Ntaganda, ambaye ni mshitakiwa wa uhalifu wa kivita
anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya ICC.
Vyanzo vya habari kutoka Idara ya Usalama vimemwambia mwandishi wa BBC
Ignatius Bahizi nchini Uganda kwamba waasi wa M23 wanadhibiti 15km wakizidi
kushika kasi kuelekea mpaka wa kusini mwa mbuga maarufu ya wanyama ya Virunga
"Virunga National Park" eneo lenye aina ya sokwe wanaishi milimani.
Wakazi wa Bunagana wanasema askari wa Kongo wamekuwa wakielekea mji wa
Kisoro, ambao ni kilometa 80 kutoka mpakani.
Msemaji wa M23 Vianney Kazarama ameliambia shirika la habari AFP kwamba waasi
wameushikilia mji huo kwa upande wa Kongo mapema siku ya Ijumaa habari ambazo
pia zimethibitishwa na wakazi wa upande wa mji huo sehemu ya Uganda .
"Waasi hao wameudhibiti mji mzima ambapo watu wote na askari wa Kongo wapo
Uganda." Chanzo cha polisi katika eneo hilo limeiambia AFP.
Karibu watu wapatao 200,000 wameyakimbia makazi yao baada ya mapigano ya hivi
karibuni nchini Kongo, ambapo pia inasadikiwa watu 20,000 wamevuka mpaka kuingia
Uganda na Rwanda.
Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitoa ripoti ikiituhumu nchi ya Rwanda
kuwaunga mkono Waasi wa Jenerali Ntaganda ambao wengi ni Watutsi ambalo ndilo
kabila la uongozi wengi wa Rwanda.
Hata hivyo nchi ya Rwanda ilikanusha madai hayo kwa nguvu zote. |
0 Comments