Sir Clement George Kahama
Na:Walusanga Ndaki
ALIINGIA katika siasa wakati viongozi wengi wa sasa nchini wakiwa bado hawajazaliwa au hawajaanza hata shule za msingi. Pia, alikuwa miongoni mwa mawaziri sita Waafrika wakati Tanganyika inapata uhuru.
Hayo hayatoshi: Alikuwa ni Mwafrika wa kwanza kuingia katika bunge la Tanganyika (wakati wa ukoloni wa Mwingereza) mwaka 1958 ambapo lilikuwa likiitwa Legico.
Ni mzee George Kahama ambaye majina yake kamili ni Sir Clement George Kahama aliyekuwa mjumbe (mbunge) wa Legico kutokea Karagwe, Jimbo la Ziwa Magharibi.
Wakati anakuwa Waziri wa Usalama na Amani ya Nchi (ambayo leo ni Wizara ya Mambo ya Ndani) mwaka 1961 Tanganyika ilivyopata uhuru, Kahama alikuwa na umri wa miaka 32, akiwa amemaliza Sekondari ya Tabora na kisha Chuo cha Loughborough cha Uingereza.
Huo ukawa mwanzo wake kuitumikia serikali kwa miaka 35 iliyofuata – hadi mwaka 1995 alipostaafu akiwa Waziri wa Vyama vya Ushirika na Masoko.
Pia, katika serikali ya muda (kabla ya uhuru) mwaka 1959, aliteuliwa kuwa Waziri wa Starehe na Maendeleo.
Kahama ambaye sasa ni mwenyekiti wa kampuni la mawasiliano ya Intanet nchini (SEACOM) amewahi kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kuendeleza Mji Mkuu (CDA), Meneja Mkuu wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Balozi huko China, na kadhalika.

Ni Sir Clement George Kahama ambaye duru za kuaminika zinasema alipewa cheo cha ‘Sir’ na Malkia wa Uingereza, miongoni mwa mambo mengine, kwa kuwa Mwafrika wa kwanza kuingia katika Legico.