STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEAS
Zanzibar
19.7.2012

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali
Mohamed Shein amewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa
misingi ya kutodhulumiana katika bei, viwango na vipimo hasa katika
mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa akisoma risala ya
Ramadhani kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa mwaka huu wa
1433 Hijriya sawa na mwaka 2012 Miladia.

Katika maelezo yake Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani ni wa neema kibiashara lakini ni vyema kufanya neema hiyo
iwe kwa wauzaji na kwa wanunuzi.

Alieleza kuwa Muuzaji anauza bidhaa zake nyingi zaidi kwa hivyo
anapaswa kuhakikisha zina ubora na anachuma faida kwa kiasi ya
anachouza.

Aidha, alisema kuwa mnunuzi naye anahitaji kupewa bei iliyo nafuu hasa
kwa bidhaa ambayo Serikali imeipunguza kodi, kwani Serikali kama
kawaida itapunguza ushuru kwa biadhaa muhimu za chakula ili
kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa bei.\

“Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa
wanasafirisha bidhaa kama vile unga, sukari na mchele walizotozwa kodi
ya chini na kuzisafirisha kwa njia ya magendo nje ya Zanzibar ili
wapate faida kubwa’,alisema Alhaj Dk. Shein.

Kutokana na mambo hayo Alhaj Dk. Shein alisema kuwa husababisha
upungufu wa baadhi ya vyakula na kuwasababishia shida wananchi wakati
huu wa mwezi wa Ramadhani.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani kwa wakulima nchini
kwa kujiandaa kuwaopa huduma nzuri wananchi hasa katika upatikanaji wa
chakula kwa ajili ya futari huku akieleza kuwa serikali imeweka
mazingira mazuri ya biashara hasa katika Mwezi huo wa Ramadhani.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nayo itajitahidi kufanya
kila linalowezekana ili kuwasaidia wananchi katika kukabiliana na
tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo mbali mbali nchini.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali imo katika juhudi za kuwaandalia
wananchi wake maisha bora, kwa kupitia mageuzi ya katiba na pia kwa
kuhesabiwa watu, mambo ambayo yamo katika sheria.


Sambamba na hayo, Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu rehema,na
kujaalia subira huku akielezea juu ya tukio la kuzama kwa meli ya MV
SKAGIT ambapo alieleza kuwa tayari maiti nyengine 22 tokea asubuhi ya
leo hadi anatoa risala yake tayari zimeokolewa.

Alhaj Dk. Shein pia, alitoa wito kwa wananchi kuwa watendaji wema na
ihsani baina yao na hasa kwa masikini na wasiojiweza ambapo utoaji
sadaka ni jambo la msingi na hakuna budi kulizingatia zaidi katika
mwezi huo wa Ramadhan ili wale wenye kipato cha chini nao uwe ni mwezi
wa furaha kwao.

Alisema kuwa kwa kuwa Ramadhani mwaka huu imekuja katika msimu wa
Watalii na ziara za Wazanzibari wanaoishi nchi za nje, inapaswa kwa
umoja wao kuonesha wema wao na mambo mema kwao na kudumisha sifa ya
ustaarabu, uvumilivu, mshikamano na kuelimishan kwa upole kwa yale
wasiyoyajua ya mila za Kizanzibari.

Aidha aliwataka wananchi wasiowajibika na saumu kama kawaida watoe
ushirikiano na wawe wastahamilivu kwa wenzano wanaofunga na wajitahidi
kutumia fursa hiyo vyema bila ya kuwakirihisha wengine.

Alhaj Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi
litaendelea kuimarisha ulizni wa watu na mali zao kwa kushirikiana na
vijana wa ulinzi shirikishi ili wananchi wapate utulivu na watekeleze
saumu kwa amani.

Dk. Shein aliwataka wazazi na walezi nao kuzisimamia vyema nyendo za
watoto wao katika mwezi huo na kuwahimiza zaidi katika ibada na darsa.
Pia, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kuutumia muda mwingi kuisoma na
kupata maarifa ya Qur-an katika Mwezi huu wa Ramadhan, mafunzo ambayo
yatadumi siku zote.

Wakati huo huo, viongozi kadhaa walifika Ikulu mjini Zanzibar kwa
ajili ya kumpa pole Dk. Shein pamoja na wananchi kwa ujumla kufuatia
ajali ya kuzama kwa meli ya MV SKAGIT na kusababisha vifo pamoja na
majeruhi.
Miongoni mwa viongozi hao ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. Mohammed Kharib Bilal pamoja na ujumbe wa Wabunge 18 wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa
Ulinzi na JKT Mhe. Shamsi Vuai Nahodha.
Rajab Mkasaba